Duru ya pili kuamua urais wa Weah Liberia

Muktasari:

Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo tangu baada ya uchaguzi wa vyama vingi kurejeshwa Waliberia kumpata rais kwa uchaguzi wa kidemokrasia.

Monrovia, Liberia. Sasa ni dhahiri kwamba mwanasoka nyota wa zamani wa Liberia George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai watachuana katika duru ya pili ya kuwania urais Novemba 7.

Wagombea wawili hao watapambana katika hatua hiyo baada ya kila mmoja kukosa asilimia 50 jumlisha moja zinazohitajika kwa mshindi kutangazwa kuwa rais.

Baada ya kuhesabiwa asilimia 95.6 ya kura 1,550,923 zilizopigwa Oktoba 10, Weah wa muungano uitwao Coalition for Democratic Change (CDC) anaongoza baada ya kupata kura 572,453 sawa na asilimia 39.0 akifuatiwa na  Boakai wa Unity Party (UP) kwenye kura 427,550 sawa na asilimia 29.1.

Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo tangu baada ya uchaguzi wa vyama vingi kurejeshwa Waliberia kumpata rais kwa uchaguzi wa kidemokrasia. Pia, itakuwa mara ya tatu kwa Weah kuwania urais tangu Liberia irejee kwenye utulivu mwaka 2003 baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 14.

Kwa mujibu wa Katiba ya Liberia, Rais na Makamu wa Rais lazima wapate kura za kutosha ili kushinda. Kura hizo nyingi inamaanisha asilimia 50+1 ya kura zote halali.

Ikiwa hakuna mgombea atakayepata kura nyingi zaidi ya nusu, ndipo uchaguzi wa marudio unaandaliwa kwa wagombea wawili wa kwanza kuamua mshindi. Hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 83 (b) ya Katiba inayoilazimisha sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuandaa uchaguzi wa duru ya pili.

Katika uchaguzi wa mwaka huu wagombea 20 walijitokeza huku Cllr. Charles Walker Brumskine wa Liberty Party (LP) akishika nafasi ya tatu baada ya kukujikusanyia kura 144,359 sawa na asilimia 9.8.