Weah aapishwa, Sirleaf akiaga Liberia

Muktasari:

Weah alishinda kinyang’anyiro cha urais kuwa mrithi wa Sirleaf baada ya kumshinda mgombea wa chama tawala Joseph Boakai katika raundi zote mbili. Kwanza aliongoza kwa asilimia 38 akifuatiwa na Boakai mwenye asilimia 28 katika uchaguzi wa Oktoba na Desemba akaibuka mshindi kwa asilimia 60.

 

 

Monrovia, Liberia. Mwanasoka nyota wa kimataifa George Weah aliyefunga ‘bao bora la urais’ katika uchaguzi wa Desemba 26, 2017 anaapishwa leo kuliongoza taifa hilo akirithi mikoba kutoka kwas mwanamama wa kwanza kura rais Ellen Johnson Sirleaf aliyemaliza muda wake.

Sherehe za kuapishwa kwa Weah, Mwanasoka wa Dunia wa Fifa 1995, pamoja na makamu wake Jewel Howard-Taylor kwenye Uwanja wa Michezo wa Samuel K. Doe (SKD). Kihistoria Weah anakuwa rais wa 24.

Baadhi ya wakuu wa nchi waliothibitisha kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake ni Jacob Zuma wa Afrika Kusini; Faure Gnassingbe wa Togo; Muhammadu Buhari wa Nigeria; Alpha Conde wa Guinea; Nana Akufo-Addo wa Ghana; Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone; Jose Mario Vaz wa Guinea Bissau; na Ali Bongo Ondimba wa Gabon.

Mbali ya wakuu wa nchi, wengine waliopata mwaliko wa kuhudhuria sherehe hizo za kihistoria ni aliyewahi kuwa meneja wake katika klabu ya Monaco ya Ufaransa, Arserne Wenger, maofisa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wanadiplomasia kutoka Marekani, Ufaransa nan chi kadhaa za Ulaya pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Maelfu ya raia wa Liberia wenye shauku ya kushuhudia tukio la kuapishwa kwa Weah, baadhi yao walikesha katika uwanja wa mpira wa taifa, mahala ambapo historia ya mwanasoka huyo inajiandika upya kutoka kung'ara katika soka na hatimaye kuingia katika uga wa siasa kuwa rais wa taifa hilo lenye historia ya milima na mabonde kisiasa.

Weah alishinda kinyang’anyiro cha urais kuwa mrithi wa Sirleaf baada ya kumshinda mgombea wa chama tawala Joseph Boakai katika raundi zote mbili. Kwanza aliongoza kwa asilimia 38 akifuatiwa na Boakai mwenye asilimia 28 katika uchaguzi wa Oktoba na Desemba akaibuka mshindi kwa asilimia 60.

Maisha ya Weah

Maisha ya Weah kuanzia utotoni yalikuwa katika mazingira duni lakini alipata mafanikio makubwa katika medani ya soka na kufanikiwa kuchezea timu kadhaa barani Ulaya ikiwemo Chelsea na AC milan. Huko ndiko alikoibuka kuwa Mwafrika pekee kuwahi kushinda Tuzo ya Mwanadoka Bora wa Fifa mwaka 1995.

Weah aliingia katika siasa baada ya kustaafu soka mwaka 2002 na akawa miongoni mwa maseneta katika bunge la Liberia. Baada ya kustaafu soka mwaka 2002 alijiingiza kwenye siasa na kwa mara ya kwanza aligombea urais mwaka 2006 lakini aliangushwa na Sirleaf.