George Weah amfukuza kazi waziri wa sheria

Muktasari:

  • Kabla ya uteuzi wake, Gibson alipatikana na hatia hiyo na Mahakama ya Juu baada ya kumtapeli mteja wake Dola za Marekani 25,000. Mahakama hiyo ilimwamuru kuzirejesha fedha hizo.

Rais mpya wa Liberia, George Weah amemfuta kazi Waziri wa Sheria, Charles Gibson baada ya malalamiko na tayari amepokonywa leseni yake ya uwakili akidaiwa kumtapeli mteja wake.

Kabla ya uteuzi wake, Gibson alipatikana na hatia hiyo na Mahakama ya Juu baada ya kumtapeli mteja wake Dola za Marekani 25,000. Mahakama hiyo ilimwamuru kuzirejesha fedha hizo.

Badala yake Rais Weah ambaye ana wiki zisizozidi tatu tangu aapishwe kuwa rais wa nchi hiyo, amefanya mabadiliko na kumteua Musa Dean aliyekuwa wakili katika Tume ya Uchaguzi kuchukua nafasi hiyo.

Mwanasoka huyo wa zamani wa Liberia alichaguliwa kuwa rais mteule wa nchi hiyo na kuapishwa Januari 22 ikiwa ni katika jaribio lake la pili toka awanie urais wa nchi hiyo. Ameweka historia kwa kuwa mwanasoka wa kwanza duniani kuchaguliwa kuwa rais.

Katika jaribio lake la kwanza Weah alichuana na Ellen Johnson Sirleaf ambaye alikuwa ndiye rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia na ambaye alikabidhi madaraka kwa amani.

Rais Sirleaf alimshinda Weah katika uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika mwaka 2005, baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa nchini humo.