Wema, mrudishe Wema yulee...

Muktasari:

Wema wa insta hapana. Huyu ndiye lakini ndiye siye.


Tunamtaka Wema wa BBM. Yule ambaye ilikuwa ngumu kumuona kibwege.

Achana na masela kina TID na Blue ambao tulisikia tu kuwa walipita kama upepo. Hata Kanumba lilikuwa jambo la ajabu kutoka na Wema.

Unaanzaje kumtokea mtoto mzuri kama yule? Achana na uzuri wake tu, alikuwa msichana mzuri mwenye taji la Miss Tanzania. Mwisho wa siku Kanumba jina lake likapaa zaidi kwa uwepo wa Wema kando ya mbavu zake.

Kanumba alikuwa staa lakini siyo ustaa wa kwenye ncha ya kilele cha ustaa wa Wema. Wema alikuwa staa na mjanja zaidi yake. Ajabu ni Kanumba kutoka na Wema. Kampataje? Wema naye kaanzaje kumkubalia?

Penzi lake lilipotuama kwa Charlz Baba siyo tu Charlz Baba alipata umaarufu zaidi, bali bendi nzima ya Twanga Pepeta ilipata umaarufu na mashabiki wengi zaidi.

Mwanzo watu walipenda mauno ya Aisha Madinda na wenzake. Uwepo wa Wema na Charlz Baba kikawa kivutio zaidi kuliko kelele za gitaa la Shakashia na tumba za MCD (R.I.P).

Diamond hakustahili kuwa na Wema kwa singo yake moja ya Nenda Kamwambie. Lakini penzi la kweli huja kabla ya mambo hayo mengine. Jina la Wema likampandisha Diamond na kuanza kutikisa kila kona ya nchi.

Wakati leo Diamond anatumika kupandisha majina ya watu mjini. Hilo jukumu Wema alilifanya miaka zaidi ya 10 nyuma. Wema yule aliwapa penzi na majina. Kwa mjanja akampa na lugha ya Kiingereza juu.

Kwa nini Wema alikuwa maarufu zaidi na kupendwa licha ya skendo zake nyingi za mapenzi? Watu aina ya Wema wapo duniani kote. Mtu anapendwa tu bila sababu. Ni karama hiyo.

Sio muigizaji mkali zaidi ya Mona au Rose Ndauka. Siyo Miss Tanzania mzuri zaidi kuliko wote waliowahi kushinda taji hilo, hapana. Lakini ukweli ni kwamba ni maarufu na anapendwa zaidi ya wenzake.

Skendo za Wema mtu mwingine angejifia au kuhama nchi. Kina Sinta hili liliwashinda wakakimbia na sanaa yenyewe. Lakini Wema hakuwahi kuyumbishwa na skendo za magazetini.

Wema aliendelea kuwa yuleyule baada ya kujiingiza kwenye sanaa ya filamu. Kama kawaida akapindua meza kibabe akawa staa huko.

Katika filamu ya Point of No Return, kuna msichana mrembo sana alionekana. Sauti yake laini pamoja na mvuto wake wa asili ulivutia wengi kumtazama, lakini kubwa zaidi lilikuwa ni umahiri wake.

Japo ilikuwa ni filamu yake ya kwanza ila alionyesha umahiri na umaridadi wa hali ya juu.

Kwa wote walioitazama ile filamu kwa mara ya kwanza walijua sanaa imepata msanii mwingine mahiri. Akawa Wema muigizaji na siyo miss mstaafu.

Hakuzungumziwa kama mshindi wa taji la Miss Tanzania aliyejawa na skendo. Ilivutia zaidi kumuita staa wa kike kwenye kiwanda cha filamu Bongo.

Tena akiitwa msanii mahiri mwenye mvuto, licha ya ugeni wake kwenye sanaa. Baada ya filamu ile na nyingine kadhaa kila kitu sasa kikabadilika.

Sanaa ina mabadiliko lakimi Wema mwenyewe amebadilika mno. Siyo Wema mwenye umahiri ule wa filamu.

Leo utasikia Wema kajibishana na watu mitandaoni, kisha kesho utaona akiposti picha ya mapaja yake.

Maisha ya Wema hii leo siyo filamu tena kama zamani, japokuwa bado anatamba na ‘taito’ ya msanii nyota wa filamu ila hilo limebaki kuwa jina tu.

Ukimtazama leo hata utembeaji wake hauna hamu wala mizuka na sanaa ya filamu. Huwezi kukisia hata kidogo kwamba Wema anataka nini zaidi kunyoshewa vidole?

Hakuna anayeweza kupinga umahiri wake kwenye kuigiza, ila pia ni uongo kusema anautendea haki.

Ni vituko na mbwembwe ndivyo vinaliweka jina lake hapo lilipo, ila kwa upande wa sanaa kuna wengi wanaweza kuzungumzwa kuliko yeye.

Kuna kitu anawanyima wapenzi wa kazi zake. Ndiyo, wanasema ana nyota kali ila watu wanapenda kuendelea kumuona na kumsikia kupitia kazi zake. Kuliko kusikia habari zake za matukio ya sherehe za ‘besidei’ na ‘arobaini’ za watoto.

Leo wakitajwa wasanii wenye kufanya vizuri wengi watamtaja Wema. Kwa sababu ya ukubwa jina lake lakini hata ukubwa wa jina na nyota ya kupendwa kwa sasa atawaachia ‘krauni’ wengine.

Muda hauna rafiki aitwaye binadamu. Kizazi cha sasa kinabadilikakila siku. Bila kupambana Wema litabaki jina kwenye droo za makumbusho. Wanaibuka kina Wema wengine wengi.

Zamani skendo zake zilishitua sana jamii. Hivi sasa ni tofauti kina Mobeto, Nandy na wenzake kina Gigy Money wanakimbiza zaidi.

Zamani ukurasa wake Insta hata kama alikosea jambo, angepambwa na kutetewa na mamilioni ya mashabiki. Leo hata asipokosea anatukanwa na kushambuliwa na mamilioni ya mashabiki.

Mvuto wake unapungua kwa kasi sana kuliko theruji ya Mlima Kilimanjaro. Zamani shabiki alifuata anachotaka.Leo anafuata anachotaka shabiki.

Kwa umahiri wake haikufaa Wema abebwe na vituko kuliko kazi zake. Wema ni mmoja kati ya mabinti wenye kuzitendea haki filamu zao. Lakini hataki kuishi kwenye msingi wa sanaa na biashara.

Sijui tatizo ni nini ameshindwa kuligeuza jina lake kuwa mamilioni ya pesa. Nguvu ya jina lake inapungua na Wema anadeka sana. Anadeka mpaka kwenye utafutaji wa pesa.

Kama mkazo ukiwa wa kweli namuona akitamba na kufanya makubwa katika filamu. Lakini siyo kwa Wema huyu. Huyu hapana, hawezi.

Udekaji wake unamponza. Muda unaenda bado anajiona mdogo. Anataka kuhimizwa na kuongozwa na watu ambao nao wanahitaji kuongozwa.

Anatakiwa kuamka na kuamua kufanya ya maana kwa kipaji chake na ukubwa wa jina kabla giza halijaingia.

Baada ya kutuonesha kila kitu kwenye maisha yake, sasa tunatamani kumuona akitisha katika filamu ndani ya ufanano wa jina lake.

Ana jina kubwa ambalo halikujengwa kupitia filamu. Msingi wa jina kupitia filamu ulishaanguka hata kabla ya Kanumba kufariki.

Tulimzungumzia Wema kifilamu siku nyingi kabla ya Lulu na Kajala hawajaonja adha ya gereza ila si sasa.

Natamani kumuona Wema akionyesha umahiri katika filamu kama nilivyowahi kumuona. Kwa sababu hakuna mchongo mwingine kwa sasa juu yake.

Sijui itatokea lini? Ila itapendeza akiamua kuachana na maisha ya maboksi na kufanya kile anachotakiwa kukifanya.

Tunasubiri kuona ukiibeba sanaa na siyo kubeba vibweka na vituko. Itapendeza ukirudi pale ulipotokea. Kwa filamu na ubora wa kucheza na kamera sio kama sasa. Lakini Kwa Wema huyu wa insta sioni maajabu labda Wema yule wa BBM.