Wema akutwa na kesi ya kujibu

Muktasari:

Mlimbwende huyo na wenzake wataanza kujitetea Mei 14 na 15, 2018


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuona msanii na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili wana kesi ya kujibu kutokana kukabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Aprili 23 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kwamba Wema na wenzake wataanza kujitetea Mei 14 na 15, 2018.

Hakimu Simba ametoa uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi watano wa upande wa mashtaka waliokuwa wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula.

Kabla ya uamuzi huo kutolewa na Hakimu Simba, Wakili Kakula aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya uamuzi kama washtakiwa hao wana kesi ya kujibu ama la.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Simba amesema kwa mujibu wa sheria iwapo washtakiwa watapatikana kuwa wana kesi ya kujibu wataanza kujitetea na wakionekana hawana kesi ya kujibu wataachiwa huru.

Hakimu Simba amesema baada ya kupitia hoja zote zilizowasilishwa mahakamani hapo imejitosheleza kwamba washtakiwa wote wana kesi ya kujibu katika mashtaka yote, hivyo wana haki ya kisheria kuanza kujitetea. 

Amesema washtakiwa wataanza kujitetea Mei 14 na 15, 2018.