KUELEKEA DODOMA: Wema itakavyowezesha kilimo cha mahindi mkoani Dodoma

Muktasari:

Mazao yanayolimwa mkoani humo ni yale yanayostahili ukame kama vile uwele, mtama, mahindi, karanga, alizeti, ufuta na zabibu.

Dodoma ni miongoni mwa mikoa iliyo na hali ya ukame kwa muda mrefu. Hupata wastani wa mvua wa milimita 500 kwa mwaka.

Mazao yanayolimwa mkoani humo ni yale yanayostahili ukame kama vile uwele, mtama, mahindi, karanga, alizeti, ufuta na zabibu.

Hata hivyo, mazao hayo kutoa zabibu, hulimwa kwa ajili ya kujikimu tu kwa njaa na siyo kibiashara, hivyo kuwafanya wakulima kuendelea kuwa masikini.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa kilimo wanasema bado kwa hali hiyo zao la mahindi linaweza kustawi kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).

Kwa Tanzania, mahindi ni zao kuu la nafaka linalolimwa katika hekta milioni mbili hadi tatu kila mwaka. Inakadiriwa kuwa kila Mtanzania hula kilo 100 za mahindi kwa mwaka.

Mahindi hutumika kupikia ugali, uji na pombe au huliwa kwa kuchomwa na pia hutumika kama chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadhiwa kama silage.

Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron), vitamini na madini mengine asilia.

Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi: punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.

Vilevile mahindi ni mabaki ya mimea na nafaka na pia hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.

Mahindi hustawi kwenye hali ya joto ambako unyevu ni wa kutosha na kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20 hadi 30.

Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua.

Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo, lakini hukua vyema zaidi katika mchanga usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Uwe na (pH) kutoka 5 hadi 8 ingawa 5.5 hadi 7 ndiyo mwafaka.

Kwa nini Dodoma?

Kutokana na hali ya hewa ya Dodoma, uzalishaji wa mahindi umekuwa mgumu. Lakini wataalamu wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Mikocheni (Mari) kupitia mradi wa Water Efficiency Maize for Africa (Wema) wanafanya utafiti ili kuwezesha zao hilo kustawi mkoani humo.

Utafiti huo unatumia mbegu zilizofanyiwa uhandisi jeni ambayo ni njia inayohusisha kubadilisha na kuboresha geni za kiumbe hai na kukifanya kuwa na tabia tofauti ili kifae kwa matumizi mengine yanayotakiwa na mhusika.

Akizungumza katika kituo cha utafiti wa Kilimo cha Makutopora mkoani Dodoma hivi karibuni, mratibu wa Wema Tanzania, Dk Aloyce Kulaya anasema wanautumia mkoa huo kwa sababu ya hali yake ya ukame ili kupata mbegu ya mahindi itakayohimili hali hiyo mahali popote Tanzania.

Katika utekelezaji mradi huo, Dk Kulaya anasema kulikuwa na awamu ya kwanza ya uchaguzi wa mbegu zinazohimili ukame (convention method) na sasa zimeshaanza kuzalishwa na kuuzwa kwa wakulima nchini.

Mradi huo unaozalisha mbegu za mahindi kwa teknolojia ya uhandisi jeni umekuwa ukitekelezwa katika nchi za Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Uganda na sasa Tanzania.

Majaribio yanaanza

Dk Kulaya anasema tayari mbegu zilizowekwa viini tete vya kuvumilia ukame na magonjwa zimetengenezwa na zitaanza kupandwa katika kituo hicho baadaye mwaka huu. Hata hivyo, kuna masharti kwa watu wanaoishi karibu na kituo hicho.

“Wananchi wanaoishi kwenye kituo hiki hawataruhusiwa kupanda mahindi ili yasije yakachavushwa na chavua kutoka kwenye majaribio. Mradi wa kwanza utachukua miaka mitatu na kila mahindi yakikomaa tunarekodi mafanikio au changamoto kisha tunayachoma ili yasitumiwe kwa chakula,” anasema na kuongeza.

“Wakati wa majaribio tutakuwa na sehemu mbili; ya kwanza tutanyunyiza milimita nane za maji kwa kila mche kwa wiki sita halafu wiki mbili zilizobaki tutakata maji. Sehemu ya pili tutanywesha maji kwa wiki zote nane.”

Ili kupata mbegu inayofaa kutumiwa na wakulima kulingana na hali ya hewa, Dk Kulaya anasema majaribio hayo yatakuwa ya kujirudia rudia hadi miaka sita, lakini hadi kupewa kibali itachukua hadi miaka 10.

Akielezea mchakato wa utafiti wa uhandisi jeni nchini, Dk Kulaya anasema walianza mwaka 2011 wakishirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (Unep) na Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Anataja sheria, kanuni na sera zinazosimamia teknolojia kuwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Bayoteki ya mwaka 2010, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 (Ema Act, 2004), Kanuni za Taifa za Usalama wa Bayoteki za mwaka 2007, Mkakati wa Kisheria wa Usalama wa Bayoteki wa mwaka 2007 na Kanuni za Kitaifa za Usalama wa Bayoteki za mwaka 2005.

Upinzani wa GMO

Licha ya kuwapo kwa sheria, kanuni na sera Dk Kulaya anakiri kuwapo upinzani kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali wakiwamo viongozi wa Serikali.

Hata hivyo, anasema upinzani huo unatokana na kutokuwa na uelewa wa teknolojia hiyo kwani madhara yote yamezingatiwa na lengo lake ni kuzalisha mazao mengi katika hali ya ukame.

“Kumekuwa na upinzani kutoka kwa watu wasiotaka teknolojia hii, hii yote ni kutokana na uelewa mdogo tu. Kwa mfano wapo wanaouliza upatikanaji wa mbegu, kwani mazao ya GMO huwa hayatoi mbegu. Ni kweli, lakini tutaandaa utaratibu wa upatikanaji wa mbegu kwa wakulima kwa bei nafuu,” anasema na kuongeza:

“Kumbuka mkulima akilima ekari moja atapata wastani wa magunia 30 ya mahindi, tofauti na mbegu za kienyeji. Kwa hiyo anaweza kufanya biashara na kupata fedha za kununulia mbegu nyingine.”

Dk Kulaya anafafanua kuwa mazao ya teknolojia hiyo huwa na utamu ule ule unaohitajika na hayana madhara yoyote kiafya.

“Wenzetu wa Kenya, Uganda, Burkina Faso na Afrika Kusini walioanza kuitumia zaidi ya miaka saba iliyopita wamefanikiwa kuongeza mazao ya kilimo na kupambana na magonjwa.

“Kwa mfano, Uganda wamefanikiwa kupambana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba ambao bado ni tatizo nchini Tanzania. Burkina Faso wanavuna tani mbili za pamba kwenye ekari moja wakati Tanzania tunaambulia kilo 200 kwenye ekari moja,” anasema Dk Kulaya.

Akizungumzia umuhimu wa teknolojia ya uhandisi jeni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko Kichocheo wa Kilimo Nyanda za Juu Kusini, Dunstan Mrutu anasema haiwezekani kwenda kwenye kilimo cha viwanda bila teknolojia hiyo.

“Tanzania ya viwanda itawezekanaje kwa kilimo hiki? Leo kila bidhaa tunaagiza nje ya nchi, kama tunataka kukuza viwanda lazima tukuze kilimo kinachotoa malighafi ya kutosha,” anasema Mrutu.