Wenye ualbino kupanda Mlima Kilimanjaro

Mkurugenzi mkazi wa taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE) yenye makao yake nchini Uholanzi, Josephat Torner.

Muktasari:

Mkurugenzi mkazi wa taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE), Josephat Torner amesema kampeni hiyo lengo lake ni kukemea imani potofu dhidi yao

Arusha. Watalii 50 wakiwemo wenye ualbino kutoka mataifa mbalimbali duniani watapanda Mlima Kilimanjaro ili kuamsha uelewa wa jamii kuondokana na imani potofu za kishirikina za kutumia viungo vya albino kupata utajiri.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Agosti 12, 2018 na mkurugenzi mkazi wa taasisi ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE) yenye makao yake nchini Uholanzi, Josephat Torner.

Amesema kampeni hiyo itasaidia kujenga jamii yenye amani inayojumuisha watu wote na kuwafanya wenye ualbino kufurahia maisha yao bila hofu.

"Kama mnavyofahamu jamii ya watu wenye ualbino barani Afrika wanaishi katika mazingira ya hofu kwa kunyimwa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, wamekua wakiwindwa kama wanyama kwa sababu za kishirikina," amesema.

Amesema licha ya Tanzania  vitendo vya kikatili dhidi ya wenye ualbino kupungua  baada ya Serikali kudhibiti hali mbaya iliyokuwepo, ameiomba Serikali kuendeleza mikakati hiyo ili kumaliza  kabisa janga hilo.

Torner amesema tayari washiriki 35 kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na 15 kutoka nchi za Afrika wamethibitisha kushiriki na kwamba washiriki kutoka Ulaya kila mmoja atatoa  Sh2 milioni zitakazosaidia taasisi hiyo kuendeleza kampeni ya kujenga uelewa.

Mratibu wa taasisi ya JTFE, Zipporah Ernest amesema upandaji mlima utafanyika Septemba 21, 2018 na kwamba watu wenye ualbino watakua 17 kati washiriki 50 ambao miongoni mwao watakuwepo madaktari wa ngozi na macho kwa ajili ya kutoa msaada pindi ukihitajika.