Watoto wenye ulemavu wasaidiwa

Muktasari:

  • Taasisi mbalimbali zimetakiwa kujitokeza kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Dar es Salaam. Taasisi ya Mitwe imepokea msaada wa vifaa kwa ajili ya watoto wenye ulemavu vyenye thamani ya Sh6 milioni.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Furaha ya nchini Uswisi, Isabella Uhlmann amekabidhi vifaa hivyo ambavyo ni viti 13, fimbo sita kwa ajili ya wasioona, baiskeli nne na bima ya afya kwa mtoto mmoja yenye thamani ya Sh50,000.

Uhlmann amesema amekuwa akifanya kazi na watu walio na ulemavu, hivyo ameguswa kutoa misaada katika taasisi kama ya Mitwe.

Amesema taasisi ya Furaha imekuwa ikifanya kazi kwa mwaka mmoja na nusu sasa, huku ikifadhili shule na taasisi mbalimbali.

"Ni wito wangu kwa taasisi nyingine kama Furaha kuja kusaidia watu wenye mahitaji maalumu," amesema Uhlmann.

Mwenyekiti wa Mitwe, Habib Hamim amesema wamefarijika kupokea msaada huo na ameomba taasisi nyingine ziige mfano ulioonyeshwa na taasisi ya Furaha.