Wenyeviti wa mitaa Mwanza walegeza, wakomaa

Muktasari:

Mlagaja amesema msimamo wao kuhusu suala hilo bado uko palepale kwamba wana haki ya kuendelea kumiliki na kutumia mihuri kuwasaidia wananchi wanaowaamini.

Mwanza. Mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa jijini Mwanza, Masasi Mlagaja amesema ingawa bado wanashikilia msimamo wa kupinga agizo la kupokonywa mihuri, baadhi wameanza kurejesha mihuri kwa watendaji.

Mlagaja amesema msimamo wao kuhusu suala hilo bado uko palepale kwamba wana haki ya kuendelea kumiliki na kutumia mihuri kuwasaidia wananchi wanaowaamini.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema mgogoro kuhusu wenyeviti kumiliki au kutomiliki mihuri umemalizwa na maelekezo ya Wizara ya Tamisemi na hivi sasa halmashauri inaendelea na utekelezaji wa agizo hilo.

“Mgogoro kuhusu mihuri umeisha, tunatekeleza agizo la Tamisemi kuhakikisha watendaji wote wanaishi kwenye mitaa yao ili kurahisisha huduma kwa wananchi wanaohitaji kugongewa mihuri kwenye nyaraka mbalimbali,” amesema Kibamba.

 

Hata hivyo Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula amekuwa akiwaunga mkono wenyeviti hao wa mitaa kupinga wasinyang’anywe mihuri yao.

Tangu Oktoba 22, mwaka jana, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza iliingia kwenye mgogoro na wenyeviti wa mitaa waligomea agizo lake la kuwataka kusalimisha mihuri kwa maofisa watendaji wa mitaa yao.