Wewe ni bilionea usiye na mtaji

Muktasari:

Sisi ni mawazo yetu. Kwa kufikiri kwetu tunakuwa kama tulivyo. Kila binadamu ni kamili na hana thamani kubwa au ndogo kuliko mwingine. Hakuna binadamu awezaye kuwa na thamani kubwa kuliko mwingine hata kama atajikweza vipi, lakini hakuna pia awezaye kuwa na thamani ndogo kuliko mwingine bila kujali anajishusha kwa kiwango gani.

Binadamu ni fikra. Ndiyo, sisi ni jinsi tunavyofikiri. Na hii ndiyo tofauti kati ya binadamu na mbuzi wala siyo miguu au manyoya.

Sisi ni mawazo yetu. Kwa kufikiri kwetu tunakuwa kama tulivyo. Kila binadamu ni kamili na hana thamani kubwa au ndogo kuliko mwingine. Hakuna binadamu awezaye kuwa na thamani kubwa kuliko mwingine hata kama atajikweza vipi, lakini hakuna pia awezaye kuwa na thamani ndogo kuliko mwingine bila kujali anajishusha kwa kiwango gani.

Kwa kuwa kila binadamu ni namna anavyofikiri ni wazi thamani ya ubinadamu wake haipo pengine popote nje yake, ambapo ni kufikiri kwake. Yale yote yaliyo nje ya binadamu hayana uwezo wa kupima thamani yake, bali yeye mwenyewe anavyofikiri na kuamini ndiyo thamani yake.

Ni kwamba thamani ya kila mmoja wetu imo ndani yake na hakuna anayeweza kuiongeza au kupunguza hadi mwenyewe anapotaka kufanya hivyo. Akiona inafaa kufanya hivyo kwa vigezo alivyonavyo.

Ni uongo kudhani binadamu anaweza kuwa vyovyote anavyotaka bila kwanza hali aitakayo kupitia kwenye fikra zake. Utofauti hujitokeza kutokana na mkondo wa fikra za mhusika.

Anayefikiri kwa njia fulani anakuwa wa namna hiyo na anayefikiri kwa njia tofauti hujitofautisha pia. Ndiyo maana huwa inasemwa ‘binadamu haaminiki.’ Kauli hii inatokana na ukweli kwamba ni vigumu kwa mtu mwingine kuujua undani wa mtu hadi pale mtu huyo atakapoona inafaa kubainisha fikra zake.

Lakini siyo kufikiri tu na kuishia hapo. Ni wazi, endapo sisi ni fikra zetu basi hatuna budi kujiuliza sisi ni wa aina gani kwa sababu kufikiri hakuko kwa aina moja.

Hii pia ndiyo tofauti kati mtu mmoja na mwingine. Kila mmoja amezaliwa na kulelewa kwenye mazingira tofauti. Kukulia kwenye mazingira tofauti kunachangia kupata uzoefu tofauti wa kimaisha.

Kutokana na sababu hizo hata kufikiri nako kutatofautiana kwani nako kwa kiasi kikubwa ni zao la mambo hayo.

Bahati mbaya tulio wengi hatujui kuwa tunafikiri kama ilivyo kupepesa macho au kupumua. Mambo ambayo ni muhimu kuyajua kwa maisha yetu. Kwa bahati mbaya huwa hatufahamu kwamba tunayafanya mpaka tukumbushwe.

Wengi wanaweza kushtuka wakati huu wanaposoma makala haya kwamba wanapumua au kupepesa macho kama ilivyo kwenye kufikiri. Watu wengi hawana habari kwamba wanafikiri hadi wakumbushwe kama sasa hivi. Kwa kuwa sisi ni kufikiri kwetu ina maana huwa hatujijui tunaishi tukiwa hatujui tunaishi.

Matokeo ya jambo hili yamejaa kila mahali. Kuna kujuta kwingi kila siku na ‘ningejua’ zisizokwisha. Kuna kukwaruzana ambako hakuna maana, kukata tamaa tunazodhani hazizuiliki au kushindwa kujua ni kwa nini tunatenda jambo fulani. Kuna kulalamika kusikoisha, hofu na mashaka.

Ni vigumu kwetu kuishi kama tunavyotaka wakati hatujajua hasa sisi ni akina nani. Tunaongozwa na miili yetu na vile vilivyo nje ya miili hiyo kwa kudhani kwamba sisi ni miili au vitu hivyo vingine.

Hebu tuchukulie kwamba tumefahamu na kukubali kwamba sisi ni kufikiri kwetu, yaani tunakuwa vile tunavyofikiri. Kama tumekubaliana na hilo, hebu tujiulize, kufikiri kwetu kukoje.

Tunaposema kufikiri kwetu kukoje, tunakuwa na maana kwamba mawazo au fikra zinazopita vichwani mwetu hutufanya tutende au kuhisi vipi na ndiyo tunakuwa sisi.

Kufikiri vizuri ni mtaji wa kuanzia. Istalahi hii ilianza kutumiwa rasmi na mtaalamu wa elimu ya mafanikio, Vicent Peal mwaka 1952 alipoandika kitabu alichokiita The Power of Positive Thinking au Nguvu ya Kufikiri Vizuri, kwa tafsiri isiyo rasmi.

Mtaalamu huyu alibainisha mifumo mikuu miwili ya kufikiri ambayo ni kufikiri vizuri na kufikiri vibaya. Bila shaka ingekuwa vigumu kwake kuandika kitabu kwa ajili ya kufundisha kufikiri vibaya kwa hiyo aliandika kitabu hicho akitaka kusaidia kufundisha watu kufikiri vizuri.

Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wengi wa elimu ya mafanikio akiwamo mwandishi wa makala haya, wamegundua kufikiri vizuri ni chanzo kikuu cha mitaji ya miradi au biashara pia mwanzo mzuri wa mafanikio.

Kufikiri vizuri ni kujaza fikra zetu kwa masuala, matukio, matarajio na picha zenye kutupa moyo, matumaini na faraja. Kufikiri vizuri ni kuondoka kwenye kuzijaza fikira zetu kwa hofu, wasiwasi na matarajio.

Tunapofikiri vizuri tunakuwa sisi ambao tumekamilika kwa sababu tunaishi kwa kadri ya utashi wetu. Kwa kuwa sisi ni jinsi tunavyofikiria kinyume na utashi wetu hatuwezi kudai kwamba tumekuwa sisi tuliokamilika.

Tunakuwa sisi tuliokamilika pale tunapofikiria kwa njia yenye kuturudisha na kutukamilisha. Anza kuwa mwanafunzi wa kufikiri vizuri kwa kuendelea mfululizo wa makala haya yanayokaribia kufika tamati.

“Ukitaka kubadilisha dunia basi badili namna ya kufikiri na ukijifunza jinsi ya kufikiri unajifunza maisha.”