Wiki ngumu kwa Waziri Kamwelwe bungeni

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe

Muktasari:

Ni baada ya kutuhumiwa na baadhi ya wabunge kuwatolea kauli za kukatisha tamaa, mwenyewe ataka wasimchonganishe na Waziri Mkuu

Dodoma. Wiki hii inayomalizika, ilikuwa ngumu kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kutokana na kunyooshewa vidole na wabunge wawili wa CCM na mmoja wa CUF kwa nyakati tofauti wakimshutumu kuwa ana majibu yasiyoridhisha yanayoonyesha jeuri.

Wabunge hao, Ramadhan Dau (Mafia - CCM); Seleman Bungara ‘Bwege’ (Kilwa Kusini - CUF) na Mohammed Mchengerwa (Rufiji - CCM) walimnyooshea kidole waziri huyo wakati wakichangia mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2019/20.

Aliyenza ni Dau ambaye Jumanne iliyopita alimtuhumu Kamwelwe akisema alizuia boti mpya isipelekwe Mafia kwa kisingizio cha kukosa abiria licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza ipelekwe.

“Tumepewa boti mpya na Bakhresa, lakini waziri huyu anakataa kuileta akitaka watu wasafiri kwa magogo, leo tunapozungumza watu zaidi ya 150 wamelala pale Nyamisati kwa kukosa usafiri,” alisema.

Dau alisema aliamua kumtumia mbunge wa viti maalumu, Hawa Mchafu ili asaidie kumshawishi waziri huyo, lakini akasema Kamwelwe aligoma akisema kama wanataka usafiri huo nauli itakuwa Sh100,000 kwa kila abiria.

Hata hivyo, waziri Kamwelwe alisema madai hayo ya Dau ni ya uongo kwani hajawahi kupinga meli kupelekwa Mafia.

Alisema Serikali ilitangaza zabuni Oktoba 24 kwa ajili ya ujenzi wa meli ya eneo hilo na kumtaka Dau asimchonganishe na Waziri Mkuu.

Jana, Mchengerwa akichangia mpango huo, alisema wakati fulani waziri Kamwelwe alikuwa akitoa kauli zisizoridhisha na za kukera.

“Sisi ni miongoni mwa watu ambao tulimpongeza sana wakati akiwa waziri wa Maji, lakini mheshimiwa Naibu Spika (Kamwelwe) amekuwa akitoa kauli wakati fulani ambazo haziridhishi,” alisema.

“Nichukue nafasi hii kumweleza ile kazi nzuri aliyoifanya wakati akiwa waziri wa maji, basi aiendeleze, yapo maeneo ambayo Rais aliweka ahadi ambazo ni sheria zinazohitaji kutekelezwa, lakini wewe mheshimiwa waziri ukinijibu kuwa uliyoachiwa na Profesa Mbarawa huhusiani nayo, napata tabu sana. Nimuombe mheshimiwa waziri ajirekebishe na arejee katika kasi yake nzuri aliyokuwa nayo wakati akiwa waziri wa maji.”

Mchengerwa aliungana na Bwege ambaye alisema Kamwelwe ana dharau.

“Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais na anathibitishwa na Bunge. Dau alimwambia habari ya boti, lakini akajibiwa majibu mabaya na waziri wa ujenzi na hii si mara moja,” alisema Bwege.

“Alikuja Kilwa akiwa naibu waziri wa maji nikamwambia kuna mradi wa maji nimeshaongea na Waziri Mkuu akanijibu Waziri Mkuu nani? Mimi namtambua Rais John Magufuli.”

Alisema, “Siyo desturi nzuri waheshimiwa, huyu ni Waziri Mkuu asidharauliwe. Nilikuwa nawaambia wabunge wa CCM jana wakasema siye tukisema sana tunaenda katika (kamati) maadili.”