Wizara haifahamu kama Polepole alizuia wafanyabiashara kulipa tozo

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph kakunda (kulia) akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe katika kikao cha 51 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda

Dodoma. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda amesema hafahamu kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alizuia utekelezaji wa sheria iliyopitishwa na baraza la madiwani wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kakunda amesema hayo leo Alhamisi Juni 14, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Kabwe Zitto.

Katika swali lake Zitto amehoji kuwa baraza la madiwani lilipitisha nyongeza za tozo na sheria ikasainiwa na waziri mwenye dhamana, lakini Polepole alizuia ma mpaka sasa watendaji wanashindwa kutekeleza jambo hilo, kutaka kauli ya Serikali kuhusu jambo hilo.

Katika majibu yake Kakunda amesema taarifa zilizopo ni kuwa baraza la madiwani lilipitisha viwango vya tozo, kwamba hata mkuu wa wilaya ana taarifa hizo.

“Hizi taarifa ambazo amezileta mheshimiwa Zitto ni mpya, hajaja ofisini kwangu, nitafuatilia kuona zina ukweli kiasi gani,” amesema.

Machi 2018, Polepole anadaiwa kuwataka wafanyabiashara wenye vibanda katika soko la Mwanga na Kigoma mjini kugomea tozo ya pango ya Sh50,000 kwa mwezi iliyopitishwa na baraza la madiwani ambalo linaongozwa na ACT Wazalendo, badala yake walipe Sh15,000 za awali.

Kufuatia kauli yake hiyo, ACT kilimtaka Polepole kuzungumzia ahadi za CCM na si kuwakataza wafanyabiashara kulipa tozo iliyopitishwa na madiwani wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.