Wizara kudhibiti vifo vya watoto njiti

Dar/Zanzibar. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya amesema Serikali inaendelea kupambana na vifo vya watoto njiti baada ya takwimu kuonyesha tatizo hilo ni la pili kusababisha vifo vingi nchini.

Takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha kati ya watoto 200,036 waliozaliwa kabla ya siku zao (njiti), 9,400 walifariki dunia kutokana na huduma duni.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti Duniani yaliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Ujerumani, Dk Mpoki alisema kukosekana kwa weledi wa kuwahudumia watoto hao wanapozaliwa na uhaba wa vifaa, huchangia vifo hivyo.

Alisema kutokana na tatizo hilo, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa kushirikiana na Ujerumani walifanya utafiti na kubaini kuwa hali ni mbaya zaidi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Gwenchele Mkenge alikiri hali ya mkoa huo ilikuwa mbaya kabla ya kuanza kwa mradi wa kuokoa maisha ya watoto njiti.

Meneja wa Mradi wa Ujerumani wa Kusaidia Afya, Dk Susanne Grimm alisema inawezekana kuokoa vifo vya watoto njiti kwa kuwa wana haki ya kuishi kama wengine.

Alisema nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanapatiwa huduma bora na stahiki.

Wakati huohuo, watoto njiti 335 wamezaliwa Zanzibar mwaka huu, ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na watoto 206 waliozaliwa mwaka 2016.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar, Moudeline Castico alisema hayo mjini Unguja jana. Alisema idadi hiyo ni kubwa, hivyo kunahitajika nguvu ya wananchi na Serikali kupitia wataalamu wa afya kutafuta njia ya kuvipunguza.