Wizara yasisitiza hakuna wanafunzi zaidi ya miaka 25 atakayechaguliwa kuingia kidato cha tano

Muktasari:

  • Akizungumza kwa simu jana, katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo alisema darasa la watoto haliwezi kuchanganywa na watu wazima.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa ufafanuzi kuhusu mwongozo wa vigezo vya udahili wa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu, hasa kipengele kilichozua utata kwamba mwanafunzi atakayedahiliwa asiwe na umri zaidi ya miaka 25 na kusisitiza msimamo huo.

Juzi, wizara hiyo ilitoa mwongozo huo wenye vigezo sita, kikiwamo hicho cha umri.

Akizungumza kwa simu jana, katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo alisema darasa la watoto haliwezi kuchanganywa na watu wazima.

“Kwenye kigezo cha umri hatuwezi kumuacha baba na mama akasoma na watoto, kwa hiyo udahili wetu utazingatia suala hilo. Mtu aliyezidi umri huo upo mfumo mwingine utakaomuwezesha kusoma na kufikia ndoto zake za kielimu,” alisema.

Aliutaja mfumo huo mwingine kuwa ni wa watahiniwa binafsi.

Dk Akwilapo alisema hata kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza upo umri wanaopaswa kuanza nao na kusisitiza kuwa waliozidi umri wa miaka 25, hawataruhusiwa kwa maelezo kuwa wanaweza kupata elimu kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (Memkwa).

“Hata kama yupo babu na bibi wanataka kuanza darasa la kwanza wataweza kupitia Memkwa lakini sio kwa darasa la kawaida lililozoeleka siku zote,” alisisitiza.

Alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa maendeleo endelevu unaosisitiza kila mtu kupata haki yake ya msingi ya elimu na hiyo ndiyo sababu inayofanya kuwa kwa mifumo isiyo rasmi ya elimu.

Vigezo vya udahili

Vigezo vipya vya udahili vilivyotajwa ni pamoja na ufaulu wa masomo yasiyopungua matatu kwa kiwango cha A, B au C katika masomo yasiyo ya dini kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

Katika mwongozo huo uliosainiwa na kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Ave Maria Semakafu, kigezo kingine ni mtahiniwa kuwa na alama za ufaulu katika masomo saba zisizozidi 25.

Pia, unataka mwanafunzi anayejiunga na kidato cha tano kuwa na alama za ufaulu kwenye masomo ya Tahasusi matatu hadi 10, pia alama F isiwe katika somo lolote la Tahasusi.

Waraka unaeleza pia kwamba wanafunzi watadahiliwa kwa ushindani kulingana na nafasi zilizopo katika shule husika kama masharti ya usajili wa shule yalivyoelekeza.

Kigezo kingine ni wanafunzi wenye sifa linganishi (ambao matokeo yao ya mitihani sio ya Baraza la Mitihani la Tanzania ), wataomba udahili kwa kutumia matokeo ambayo yamefanyiwa ulinganifu.

Hakielimu watoa neno

Ofisa Programu, Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera taasisi ya HakiElimu, Florige Lyelu alisema kwa kuwa kuna watahiniwa binafsi kwa masomo ya kidato cha nne, kigezo hicho sio sahihi.

“Mnajua wazi kuna QT (mtihani wa maarifa) ambao upo kisheria sasa hawa wanapomaliza na kufaulu waende wapi? Hiki kigezo sio sahihi lakini pia miongozo hii inayotolewa ni vizuri ingekuwa inashirikisha maoni ya wadau wa elimu,” alisema.

Lyelu alisema ili kusiwe na miongozi mingi kwenye elimu, lazima iundwe sera itakayokuwa kama katiba ambayo, haitawafanya wateule wapya kufumua na kuweka wanayofikiri yanafaa huku wakija wengine wanaondoa.

“Mfano suala la maswali ya kujieleza ambalo ni muhimu, liliondolewa kwenye mitihani lakini juzi tena limerudishwa. Sasa tunashindwa kuelewa kwa nini liondolewe na kurudishwa, tunahitaji sera itakayokuwa kama katiba ili kila atakayeingia aitekeleze hiyo,” alisisitiza.