Wizara zagonga mwamba Udom

Muktasari:

Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula jana alithibitisha kupokea maombi kutoka kwa wizara hizo.

Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kimekataa maombi kutoka kwa wizara mbili ya kutumia baadhi ya majengo yake kwa ajili ya ofisi pindi Serikali itakapohamishia makao makuu rasmi mjini hapa, ili kulinda hadhi na taaluma kwa wanafunzi.

Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula jana alithibitisha kupokea maombi kutoka kwa wizara hizo.

“Kwa kusema kweli nimetembea karibu dunia nzima, lakini kwa uzoefu wangu sijawahi kuona mahali popote ambapo Serikali inakaa ndani ya eneo la chuo kikuu,” alisema bila ya kuzitaja wizara hizo.

Profesa Kikula alisema kulingana na maadili ya kitaaluma, haiwezekani Serikali kukaa pamoja na chuo kikuu kwani hali kama hiyo itaathiri shughuli za kielimu.

Alisema hajakataa maombi ya wizara hizo kwa ajili ya sababu za kisiasa, bali ameangalia zaidi umuhimu wa kulinda hadhi na heshima ya chuo hicho ambacho kimekuwa kikizalisha wataalamu makini wanaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na teknolojia nchini.

“Binafsi nimefurahi sana msimamo wa Rais John Magufuli wa kuhamishia Serikali Dodoma, lakini siwezi kuruhusu wizara yoyote kutumia majengo yetu japo chuo hiki ni cha Serikali pia,” alisema na kuongeza: “Kwa mfano, fikiria, ukiruhusu wizara kama ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kukaa hapa nini unachotegemea zaidi ya migogoro ya mara kwa mara ya wanafunzi kuvamia wizara hiyo kipindi cha ucheleweshaji wa mahitaji yao?” alihoji.

Tangu Rais Magufuli atangaze rasmi msimamo wake wa kuhamishia Serikali Dodoma, wizara nyingi na idara zake zimekuwa katika hekaheka za kutafuta nafasi katika majengo mbalimbali kwa ajili ya ofisi.