Yanayochangia umasikini Afrika haya hapa

Muktasari:

Vyama vya siasa vina nguvu kubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi Afrika

Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa wamebainisha mambo manne yanayochangia umasikini Afrika.

Mambo hayo yametajwa kuwa mipango inayotegemea misaada ya nje na yenye masharti magumu; migogoro ya wenyewe kwa wenyewe; kukithiri kwa rushwa na uvunjifu wa haki za binadamu.

Hayo yamesemwa kwenye mkutano unaovikutanisha vyama vya siasa zaidi ya 40 vya Afrika na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Washiriki wa mkutano huo unaofanyika leo Julai 18, 2018 wanajadili namna ya kuanzisha ushirikiano mpya wenye tija baina yao.

Katibu mkuu wa vyama vya siasa Afrika, Najie Ally Najie amesema hakuna namna Afrika inaweza kuufikia uchumi wa kati bila kuondokana na changamoto hizo.

Amesema ili nchi yoyote iendelee lazima ikubali kufanya mabadiliko makubwa na kuwa na utawala unaoongoza kwa haki, maadili na unaolenga kutatua matatizo ya wananchi.

"Huu ni wakati muafaka wa kuimarisha uhusiano wetu Afrika lakini pia na uhusiano baina yetu na China," alisema.

Kiongozi wa CNDD-FDD kutoka Burundi, Evarist Ndeyishimye amesema makubaliano ya vyama vya siasa vya Afrika ni kuimarisha umoja utakaosaidia kuondokana na changamoto zilizopo.

"China haikujengwa kwa siku moja vivyo hivyo kwa Afrika, haitajengwa siku moja," alisema.

Ndeyishimye amesema uzoefu wa CPC uwe chachu kwa Afrika katika kupiga hatua kimaendeleo na kujinasua katika wimbi la umaskini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema mkutano huo ni mwanzo wa uhusiano imara na wenye tija kwa Afrika na China.

"Unapotaka kutoa uongozi kwa watu lazima uwe na taasisi imara. Vyama vya siasa vina nguvu kubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi Afrika, mkutano huu umetukumbusha nidhamu ya viongozi wa siasa itafanya tufikie ndoto yetu kiuchumi," alisema.