Young Dee asema alipikwa na Pancho Latino

Msanii wa Bongo Fleva, David Genzi maarufu ‘Young Dee’.

Muktasari:

  • Amesema Dully Sykes aliyekuwa akimsimamia alimkabidhi kwa Pancho Latino akae naye mwaka mzima ili kumpika kimuziki.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, David Genzi maarufu ‘Young Dee’, amesema kabla ya kutoka kimuziki alikaa na mtayarishaji wa muziki nchini Joshua Magawa 'Pancho Latino' kwa mwaka mzima akimpika kimuziki.

Pancho aliyefariki juzi baada ya kupata mkasa wa kuzama katika kisiwa cha Mbudya akiwa anaogelea, aliwahi kufanya kazi katika studio mbalimbali ikiwemo ya Dhahabu Records inayomilikiwa na Dully Sykes.

Amesema tangu alipokabidhiwa kwake alihakikisha anakaa naye takribani mwaka mzima kumpika kimuziki na anashukuru  hata baada ya kutoa wimbo wake wa kwanza wa Tafsiri alipokelewa vizuri na mashabiki.

“Nilikabidhiwa kwake na Dully Sykes na kujikuta napata ‘interview’ nyingi kutoka kwa vyombo mbalimbali vya habari na hapo ndio ikawa mwanzo wangu wa kujulikana,” amesema.

Amesema mafanikio yake ya kimuziki kamwe hawezi kuacha kuyazungumzia bila kumtaja Pancho kwani ni mtayarishaji aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu cha kuwatengeneza wasanii.

“Yaani mpaka sasa siamini kwamba Pancho ametutoka,”amesema Young Dee.