ZFDA yateketeza tani 20 za maziwa yaliyoharibika, yawashauri wafanyabiashara kuzingatia sheria

Muktasari:

  • Akizungumza wakati wa kuteketeza maziwa hayo juzi, kaimu mkurugenzi Idara ya Udhibiti wa Chakula na Dawa, Dk Khamis Ali Omar alisema maziwa hayo yaliingizwa Zanzibar yakitokea Dubai huku yakiwa yamepakiwa katika kontena yakichanganywa na mizigo mingine ikiwamo gari.

Zanzibar. Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) imeteketeza tani 20 za maziwa yaliyoharibika, huku ikiwataka wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za chakula kuzingatia miongozo, sheria na kanuni.

Akizungumza wakati wa kuteketeza maziwa hayo juzi, kaimu mkurugenzi Idara ya Udhibiti wa Chakula na Dawa, Dk Khamis Ali Omar alisema maziwa hayo yaliingizwa Zanzibar yakitokea Dubai huku yakiwa yamepakiwa katika kontena yakichanganywa na mizigo mingine ikiwamo gari.

Dk Khamis alibainisha kuwa maziwa hayo yaliharibika kutokana na baadhi ya maboksi kupasuka na kumwagika, hivyo kusababisha mengine kulowana.

Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia njia nzuri kusafirisha bidhaa zao ili kuepuka hasara na kuwalinda walaji wa bidhaa zao.

Maziwa hayo yaliingizwa nchini Juni 6 na Essak Suleiman, lakini mamlaka hiyo iliyazuia kabla ya kuingiza sokoni.

Naye mkuu wa kitengo cha uchambuzi wa athari zitokanazo na chakula wa ZFDA, Asha Suleiman aliwashauri wananchi wanapokuwa na mashaka na chakula na kuhisi kina dalili ya kuharibika kutoa taarifa mapema.

Akizungumzia hali hiyo, Suleiman alisema sababu ya maziwa hayo kuharibika ni upakiaji mbaya uliofanywa na wamiliki wa meli na chombo hicho kuchelewa kuondoka Dubai.