Zaidi ya Sh1.1 bilioni kupeleka maji Kibondo

Muktasari:

  • Akijibu swali la Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye, leo (Jumatano), waziri huyo amesema Sh300 milioni zitatumika kupanua mtandao wa maji kwa kilomita saba na ukarabati wa bomba la maji urefu wa kilomita nne na ufungaji wa pampu.

 Baada ya chanzo kilichokuwapo kuharibika, Serikali imetenga zaidi ya Sh1.1 bilioni ili kuboresha huduma ya maji wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaac Kamwela amesema fedha hizo zitatolewa kwenye mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai Mosi.

Akijibu swali la Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye, leo (Jumatano), waziri huyo amesema Sh300 milioni zitatumika kupanua mtandao wa maji kwa kilomita saba na ukarabati wa bomba la maji urefu wa kilomita nne na ufungaji wa pampu.

Licha ya fedha hizo, Mhandisi Kamwela amesema ili kuhakikisha wananchi wa Kibondo wanapata maji safi na salama, amesema: "Serikali imetenga Sh826.8 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini."

Mhandisi Nditiye alitaka kujua mpango wa serikali kutafuta chanzo kingine cha maji baada ya kilichopo kuharibiwa na shughuli za binadamu.