Tuesday, January 9, 2018

Zanzibar wajizatiti kuzalisha sukari yao, tatizo soko

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Licha ya udogo wake ki eneo, visiwa vya Unguja na Pemba vimekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa sukari ya kutosheleza mahitaji ya wananchi zaidi ya milioni moja.

Zanzibar imekuwa ikitumia kati ya tani 17,000 hadi 20,000 za sukari kwa mwaka, huku sehemu kubwa ya sukari inayotumika visiwani humo ikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Tangu miaka ya 1970 Zanzibar ilikuwa na kiwanda cha sukari kilichopo eneo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja kilichokuwa kikimiliwa na Serikiali.

Hata hivyo baada ya miaka sita, Serikali ilishindwa kukiendesha, hivyo uzalishaji wa sukari ukakwama mwaka 1978.

Baada ya miaka 35, Kampuni ya Export Trading Group ilikichukua kiwanda hicho na kuanza kukifufua kwa kufunga mashine mpya za kuchakata na kuzalisha sukari. Hiyo ndiyo Zanzibar Sugar Factory Limited.

Meneja wa kiwanda hicho, Rajesh Kumar anasema ukarabati wa kiwanda hicho umechukua miaka mitatu katika eneo la uchakataji, uzalishaji wa umeme na sehemu ya utengenezaji wa spirit ‘distillation’.

Vilevile kampuni hiyo imeongeza mashamba ya miwa na kuanziswha utaratibu mpya wa wakulima wa nje.

“Uzalishaji wa kwanza wa sukari umeanza Machi 2016 baada ya matengenezo hayo.

INAENDELEA UK 24


iNATOKA UK23

Tulizalisha kwa mwezi mmoja kisha tukasitisha ili kujipanga zaidi. Tuliendelea na uzalishaji Julai, Agosti, Septemba na Oktoba (tukapata) tani 4,805,” anasema Kumar.

Baada ya hapo walifanya tena ukarabati wa mitambo, hadi Julai mwaka 2017 walipoanza uzalishaji wa sukari, lengo likiwa ni kuzalisha tani 5,600 za sukari hadi mwisho wa mwaka 2017.

Mbali na kuzalisha sukari, kiwanda hicho kinatumia mabaki ya miwa (molasses) kuzalisha umeme megawati tatu zinazotosha kuendesha mitambo na kiwanda kwa ujumla, japo pia hutumia umeme wa Shirika la Zeco.

Kumar anasema kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 235 walioajiriwa moja kwa moja na wanawahudumia hata kama kiwanda kimefungwa.

Msimamizi wa mashamba ya miwa ya kampuni hiyo, Khamis Omari Ameir anasema kwa sasa wana mashamba yenye ukubwa wa ekari 3,099 lakini wanatarajia kuwa na mashamba yenye ukubwa wa ekari 7,000 yakihusisha pia mashamba ya wakulima wadogo.

Anasema mbali na mashamba hayo, kuna wakulima wadogo (outgrowers) wapatao 450 wanaowahudumia kwa kuwapatia pembejeo kama viutilifu, mbolea, mbegu pamoja na kulima na kuvuna.

“Mbegu zetu zinatumia mwaka mmoja hadi kuvunwa, mwaka huu tumevuna tani 1,300 kutoka kwa wakulima wadogo na tunategemea mavuno yataongezeka,” anasema.

Anasema mkulima huwauzia tani moja kati ya Sh45,000 hadi Sh55,000, hivyo mkulima hupata kipato kikubwa kulingana na eneo alilo nalo.

Baadhi ya wakulima wadogo waliozungumza na gazeti hili wanasema bado wanajifunza kilimo cha miwa ya sukari.

Pembe Khamis anayeishi Kijiji cha Kilombero anasema analima ekari mbili na nusu ya miwa ambapo kwa mara ya kwanza alipata tani 55 na baada ya kuuza katika kiwanda hicho alilipwa Sh9.6 milioni na bado anadai Sh1.5.

“Tatizo la Zanzibar ni uhaba wa ardhi kiasi kwamba kwa shamba langu siwezi kupata mavuno mengi. Tatizo miwa hii ni kwa ajili ya sukari tu, huwezi kukata na kwenda kuuza mitaani, kwa hiyo unapolima ni lazima usubiri mwaka mzima ikomae ukauze kiwandani, siyo vinginevyo. Tunawashukuru ZSFL kwa kutupa mafunzo, pembejeo na kutulimia,” anasema Khamis.

Naye Abdallah Said anayetoka Kijiji cha Bubwisudi anasema alianza na shamba la ekari tatu na sasa ana ekari 11 za miwa.

“Tatizo kubwa kwangu ni wizi wa miwa unaofanywa na majirani, lakini kwa kiasi fulani biashara inakwenda vizuri,” anasema Said.

Jinsi sukari inavyotengenezwa

Akieleza mchakato wa utengenezaji wa sukari, ofisa rasilimali watu wa kiwanda hicho, Khamis Haji anasema miwa ikitoka shambani hupitia katika mizani kupimwa ili kujua wingi wake unapelekwa kwenye mashine maalum inayokata ili kupunguza ukubwa wake ili uingizwe kwenye mtambo wa kukamua.

Mkemia mkuu msaidizi wa kiwanda hicho, Herman Mhongobola anasema baada ya miwa kukamuliwa, juisi yake hupelekwa kuchakatwa kwa kupitia hatua kadhaa ikiwa pamoja na kuchemshwa ili kuua vidudu na kutoa hewa kwa kuchanganya na chokaa.

“Baada ya kuchemsha katika nyuzijoto 103, inachanganywa na chokaa, ambayo hubakiza matope chini na juisi nzuri juu. Juisi hiyo huchemshwa ili kutoa maji na kubakiza utamu tu. Uchemshwaji huendelea hadi zinapopatikana mchanganyiko wa sukari na molasses,” anafafanua Mhongobola.

Anasema baada ya hapo mchanganyiko huo hupelekwa kwenye mtambo wa kutenganisha sukari na molasses. Baada ya hapo sukari hukaushwa na kwenda kuwekwa kwenye mifuko.

“Hakuna kemikali inayoongezwa kwenye sukari yetu. Chokaa inayowekwa ni kwa ajili ya kutrenganisha juisi na matope na kurahisisha uchemshaji. Kwa mchakato wote huo, asilimia 15 tu ndiyo sukari na asilimia 85 ni maji,” anasema Mhongobola.

Tatizo la masoko

Meneja mkuu wa kiwanda hicho, Rajesh Kumar anasema licha ya kuzalisha sukari kwa gharama kubwa wanapata hasara kwa kulikosa soko la Bara.

“Tunahitaji kuuza sukari yetu Bara ambako ni Sh95,000 hadi Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50, lakini hapa ni Sh60,000 hadi Sh70,000. Tumekuwa tukijadiliana na Waziri wa Biashara ili kutusaidia kupata soko la Bara.

“Tunajiuliza kama hii ni Tanzania moja na hata baadhi ya vifaa tunavyotumia kama mifuko ya sukari inatoka, Dar es Salaam, lakini haturuhusiwi kuuza sukari tu Bara,” anasema Kumar.

Anasema kiwanda hicho kimeajiri rasmi watu 235 mbali na ajira zisizo rasmi na kina mitambo ya kisasa hivyo wanahitaji masoko ya uhakika hasa Bara.

“Kwa hiyo ni lazima tuuze sukari ili kiwanda kiendelee. Hiki ni kiwanda pekee na kikubwa Zanzibar cha sukari, tumeajiri wafanyakazi zaidi ya 235 hivyo tunahitaji msaada wa Serikali ili tuendelee,” anasema Kumar.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amelalamikia katazo la Serikali ya Muungano kuzuia sukari inayozalishwa Zanzibar kuuzwa Bara akisema ni kinyume na matakwa ya Muungano na matakwa ya soko.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Zanzibar hivi karibuni, Balozi Amina anasema wamekuwa na majadiliano na Serikali ya Muungano kuhusu kadhia hiyo ambayo yataendelea mwisho wa mwezi huu.

Akizungumzia kadhia hiyo, Balozi Amina anasema licha ya ukweli kwamba sukari inayozalishwa na kiwanda pekee cha Zanzibar Sugar Factory Ltd haitoshelezi mahitaji ya Wazanzibari bado wana haki ya kuuza popote wanapotaka.

“Mimi kama Waziri wa Biashara na Viwanda niliona tuwe na ‘combination’, kwamba sehemu wauze Zanzibar na nyingine wauze Bara, lakini Serikali ya Muungano haitaki kununua sukari kutoka Zanzibar. Sasa hilo nilitaka tuzungumze, kwa sababu siyo fair (sawa),” anasema Balozi Amina na kuongeza:

“Arguments’ (hoja) kwamba haitoshelezi soko la Zanzibar si sahihi. Kwa sababu kama kiwanda kipo na kina zalisha, wana right (haki) ya kuuza Zanzibar au wakauza Bara. Kwa sababu kama ni hivyo kuna viwanda vya Bara vinauza Zanzibar lakini havijatosheleza soko la Bara, kwa sababu hili soko liko ‘free’ (huru) mtu anatakiwa ku ‘access’ (kupata) soko kama anavyoona ni sawa.”

Waziri Amina aliyewahi kuwa Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani anasema madai kuwa Zanzibar haina kiwanda cha sukari na kwamba sukari hiyo inaagizwa kutoka nje ya nchi hayana msingi kwa kuwa kiwanda kipo na kimeshatembelewa na viongozi wakiwemo wa Serikali ya Muungano.

“Kwa hiyo wanapotuambia haiwezi kuuzwa bara kwa sababu haitoshelezi Zanzibar, that’s not right (siyo haki). Kwa sababu ‘fundamentally’ (kimsingi) huko ni kwenda kinyume na misingi ya soko na misingi ya huu muungano wetu,” anasema.

-->