Ziara ya Ndalichako KIU yanasa raia wa kigeni 30 wasio na vibali

Muktasari:

Ugeni huo uliongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyeambatana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa.

 Wahenga wana msemo; mgeni njoo, mwenyeji apone. Lakini ugeni wa jana uliokuwa wa ghafla wa viongozi waandamizi wa Serikali katika Chuo Kikuu cha Kampala (KIU), tawi la Dar es Salaam uligeuka shubiri kwa wenyeji baada ya watumishi 30 wa chuo hicho kukamatwa wakidaiwa kufanya kazi nchini bila ya kuwa na vibali vya kazi.

Ugeni huo uliongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyeambatana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa.

Akizungumzia kukamatwa kwa wageni hao, Dk Makakala alisema chuo hicho kimekuwa hakitoi ushirikiano kila maofisa kutoka Uhamiaji wanapofika kufanya ukaguzi na kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakikimbia na kuruka ukuta kitendo kilichoashiria kutokuwapo uhalali wa wao kuwa nchini.

“Nimshukuru Waziri wa Elimu kwa kutushirikisha kwenye ziara hii, kazi itakuwa endelevu kwa kushirikiana ili kubaini wote wanaoishi nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria,” alisema Dk Makakala.

Profesa Ndalichako alisema chuo hicho kimekuwa kikikabiliwa na kashfa nyingi ikiwamo kuajiri watu wasiokuwa na sifa ya kutoa huduma za elimu na wengine wamekuwa wakituhumiwa kujishughulisha na biashara haramu.

“Wapo raia wengi wa kigeni wameingia kama wanafunzi na wengine kwa ajili ya matembezi lakini leo cha kushangaza wamekuwa ni waajiriwa wa chuo hiki, huku Watanzania wakiwa madereva na wafanya usafi,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho wameajiriwa zaidi ya sehemu moja jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya viongozi wa umma.

“Wapo walioingia nchini kama wanafunzi lakini baada ya muda wakaajiriwa kama wafanyakazi. Hii kwa sheria za nchi haikubaliki lakini wapo wafanyakazi wa Serikali ambao wameajiriwa lakini kwenye ukaguzi niliofanya wanaonyesha kuwa ni waajiriwa hapa,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri aliwataja baadhi ya waajiriwa wa umma waliokutwa wameajiriwa chuoni hapo ambao alisema ni kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Ripoti iliyowasilishwa kwa waziri imeonyesha kuwa kuna wafanyakazi wanaofanya kazi chuoni hapo ambao ni raia wa kigeni baadhi yao wamekuwa wakiishi nchini bila kibali kutoka Idara ya Uhamiaji.

Ripoti hiyo inaonyesha raia wa kigeni kutoka Nigeria ni 29; Uganda 48 na Kenya 16.