Zitambue tabia za mtu mwenye dalili ya usonji

“Huyu mtoto ni msumbufu sana, ana hasira, muharibifu, mchoyo, mbinafsi, mzito kuelewa, anapenda sana kujiumiza, sio msikivu, anapenda kurukaruka na kufanya vitendo vingine vya kushangaza.”

Haya ni baadhi tu ya mambo machache ambayo, mama au ndugu wa mtoto mwenye usonji anaweza kuyasema pindi anapozungumza na mtu mwingine au daktari au hata mtaalamu mwingine wa afya.

Haya yote husemwa kutokana na wazazi, walezi na hata jamii, kutokana na wao kushindwa kutambua na kutafsiri tabia za watoto wenye tatizo hilo la usonji.

Wataalamu wa afya na madaktari wanasema, kukosekana kwa elimu ya utambuzi kwa jamii kuhusiana na ugonjwa wa usonji, kunasababisha watu hawa kukosa huduma muhimu za afya zinazoweza kuwafanya waweze kujitegemea.

Wengi wao huachwa kiasi cha kuwafanya wawe tegemezi kwa kila kitu na kuathirika kisaikolojia.

Usonji ni nini?

Usonji ni ugonjwa ambao huanza kutambulika kwa mtoto akiwa na miaka kati ya miwili na mitatu.

Ili uweze kumtambua mtoto mwenye usonji, zipo dalili zinazoonyeshwa na mtoto huyo.

Miongoni mwa tabia hizo ni pamoja na kushindwa kuonyesha uwezo wake wa kuelewa na kutafsiri hisia za watu wengine.

Wataalamu wa afya wanasema mtoto mwenye usonji anaweza kuwa na upungufu kwenye kutambua hali ya kukasirika inayoonyeshwa na mtu mwingine.

Wanasema jambo hilo linaweza kuonekana na wengine kuwa huenda mtoto huyo ana dharau, mtukutu au hajali kitu.

Mtoto mwenye usonji mara nyingi hupendelea kucheza peke yake, hapendi kushirikiana na wengine.

Na hata akishirikiana na akishirikiana na watoto wenzake bado uwezo wake unakuwa wa kiwango cha chini ambao hauwezi kumuwezesha kuwaruhusu wenzake hao watumie au kuchezea vitu vyake.

Hali kama hii, ndiyo mara nyingi huwafanya watu wamchukulie kuwa ni mchoyo.

Aina ya michezo wanayoipendelea

Mtoto mwenye usonji mara zote hupenda kucheza michezo inayojirudia mfano ule wa kujizungusha au kuchezesha kichwa au sehemu moja ya mwili au wakati mwingine hupendelea kuchezea aina fulani ya kifaa anachokuwa nacho muda wote.

Mawasiliano

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema mara nyingi watoto hawa huwa na tatizo la kutafsiri lugha ya maneno na ishara.

Tatizo hilo huwasababishia tatizo la kujifunza na kutumia lugha wawapo nyumbani, shuleni au katika maeneo ya michezo yao awapo na watoto wenzake

Kutokana na tatizo la kushindwa kujieleza, wanajikuta wanashikwa na hasira hasa wanapotaka kitu fulani.

Hali hiyo humsababishia ukali na kujikuta akiwapiga wenzake, kulia sana, kuvunja vitu na hata kujijeruhi mwenyewe.

Tabia anazoweza kuwa nazo mtoto mwenye usonji

Watoto hawa hupendelea kuonyesha tabia zinazotabirika. Na hii inaonekana zaidi katika ratiba zao za kila siku.

Jambo hili huwafanya wapate shida pale ratiba ya kitu fulani inapobadilika.

“Kama akiamka asubuhi huanza na kusafisha kinywa, anywe chai ndipo avae sare ya shule, atataka ratiba hiyo iwe hivyo isibadilishwe.”

Kama itabadilishwa itampatia wakati mgumu kuimudu. Pia, watoto hawa hupendelea mazingira yasiyobadilika.

Kama anapenda kucheza nje ya nyumbani kwao, siku zote utamkuta akicheza hapo na kama hupendelea kukalia kochi moja sebleni, daima atalitumia hilo kila akaapo sebleni, na mtu mwingine akilikalia huwa ugomvi.

Wakati mwine mtoto wa aina hii hukosa uwezo wa kutulia sehemu moja na mara nyingi hupenda kukimbiakimbia na kurukaruka kwenye makochi, vitanda na hata katika vibaraza.

Madaktari wanasema kushindwa huko kutulia ni sehemu moja kunasababisha mtoto huyo ashindwe kujifunza mambo mengi.

Kutokana na kuwa na changamoto katika maeneo tajwa hapo juu, mtu mwenye usonji utendaji wake huathirika zaidi kukosa uwezo wa kujitegemea katika mambo mengi kama ilivyo kwa watoto wenye rika sawa na lake.

“Mara nyingi hushindwa kujitegemea katika kujifanyia usafi binafsi wa mwili hususani masuala ya msalani, kula na kupendelea kuvaa aina moja tu ya nguo.” Anaweza pia kuwa na tatizo la kujifunza masomo ya darasani na changamoto ya kujenga uhusiano kadiri ya rika, katika umri wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Dk Godfrey Kimathy ni mtaalamu wa tiba kwa vitendo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Waweza kuwasiliana naye kwa simu ya kiganjani namba 0622 78 6859