Zitto, Serukamba wakabana koo Muswada wa Habari

File Photo

Muktasari:

Wawili hao ambao ni marafiki tangu utotoni na walibadilishana majimbo mkoani Kigoma, walijikuta wakilumbana kutokana na kupishana kimtazamo kuhusu utolewaji huo wa maoni.

Dodoma. Mvutano mkali uliibuka jana kati ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba (CCM) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) kuhusu kupokea maoni ya wadau katika Muswada wa Sheria wa Huduma za Habari Mwaka 2016.

Wawili hao ambao ni marafiki tangu utotoni na walibadilishana majimbo mkoani Kigoma, walijikuta wakilumbana kutokana na kupishana kimtazamo kuhusu utolewaji huo wa maoni.

Zitto alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) kabla ya uchaguzi wa 2015 na Serukamba alikuwa Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM) kabla ya uchaguzi huo, lakini katika uchaguzi wa mwaka jana, Zitto aligombea Jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo na Serukamba aligombea Kigoma Kaskazini kupitia CCM na wote walishinda.

Jana, kamati inayoongozwa na Serukamba ilikuwa ikipokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo lakini wadau saba waliofika kutoa maoni yao, wote waliomba muda zaidi ili kuupitia.

Hali ilichafuka baada ya Serukamba kusoma maudhui ya sheria hiyo pamoja na mchakato wake katika hatua zote, na baada ya kumaliza kusoma akataka wadau waanze kutoa maoni yao hali iliyomuibua Zitto.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hapa yupo Waziri mhusika (Nape Nnauye) ningependa atusaidie kujua kama wadau walipata muda wa kushirikishwa kikamilifu na kuwapa nafasi nzuri ya kutoa maoni yao,” alihoji Zitto.

Kauli ya mbunge huyo ilipokewa kwa zogo na wabunge ambao wengi waliunga mkono, lakini baadhi wakaipinga huku wakiendeleza zogo ndani ya ukumbi.

Serukamba aliyekuwa akisisitiza kuwa yuko sahihi kuhusu namna ya uendeshaji wa vikao, alijikuta akipingwa na kila mtu hata akaanza kumlalamikia Zitto kuwa anasimama upande wa wadau wakati yeye ni mbunge, ndipo mbunge huyo akajibu kwa sauti kuwa wapo wapigakura wake kutoka Kigoma Mjini wanaohusika na muswada huo.

Nafasi ilikwenda kwa Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia ambaye aliungana na Zitto na kusema; “jana (juzi) Waziri alikuja hapa na kusoma taarifa yake kisha akaondoka na hatukuwa na muda wa kuhoji, leo tena mwenyekiti unataka kufanya hivyo, hii haiwezekani.”

Mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Jasmin Tsekwa walipinga kauli ya Zitto kuwa ilipaswa kuulizwa siku moja kabla ya kikao, kauli zilizoongeza zogo na mabishano kutoka kundi kubwa la wabunge wakitaka wabunge hao wasiwe sehemu ya Serikali.

Baada ya kuona hali imekuwa ngumu, Serukamba aliteta kidogo na Waziri Nape kisha akaomba wadau na waandishi wa habari watoke nje kwa muda kabla ya kuwaita tena.

Waliporejea, alianza kuwaita moja kwa moja wadau kutoa maoni yao akianza na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), ambapo katibu wao Henry Muhanika alisema hawajashirikishwa na kuomba wapewe muda zaidi.

Baraza la Habari Tanzania (MCT), waliowakilishwa na Pili Mtambalike, Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kupitia kwa Makamu wa Rais, Jane Mihanji, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kupitia kwa Deodatus Balile na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka wote waliomba kupewa muda hadi Februari mwakani.

Wengine walioshiriki na kuomba muda uongezwe ni MisaTan, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Nola ambao walitetea kuwa hawakupata muda wa kujadili zaidi.

Hata hivyo, Serukamba alipandisha sauti na kuwataka kuangalia namna ambavyo wanatakiwa kufanya kwa kuwa Serikali ilishawapa nafasi na vielelezo vinaonyesha hivyo. “Sasa kama hakuna mtu mwenye maoni tofauti, basi hakuna sababu tena na kuendelea naomba mtoke ili sisi tuendelee na mchakato wetu,” alisema Serukamba na kuwatoa nje wadau hao na wanahabari.

Mbali na juhudi zote hizo, zogo lilikuwa kubwa ndani ya ukumbi huo hali iliyomlazimu Serukamba kuahirisha kikao hicho hadi leo. Baadaye Serukamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa anatoa wiki moja kwa wadau wote kupeleka maoni yao kwa maandishi.