Zitto Kabwe: Kama ningepata mamlaka ningefanya tofauti

Muktasari:

  • Siku chache zilizopita, nilijipa muda huo wa utulivu kwa ajili ya tafakari. Swali kuu nililokuwa nikijiuliza ni hili; kwamba kama ningekuwa nimepewa mamlaka ya kuongoza Tanzania nini ningefanya tofauti na wanaoongoza sasa?

Kwa miaka mingi nimekuwa mtu ninayeamini katika kujipa muda wa upweke na kutazama dunia iliyonizunguka na kujiuliza maswali ama kunihusu mimi binafsi, au kuhusu nchi yangu na Afrika.

Siku chache zilizopita, nilijipa muda huo wa utulivu kwa ajili ya tafakari. Swali kuu nililokuwa nikijiuliza ni hili; kwamba kama ningekuwa nimepewa mamlaka ya kuongoza Tanzania nini ningefanya tofauti na wanaoongoza sasa?

Hitimisho la tafakuri yangu likaangukia wilayani Ludewa mkoani Njombe. Kwenye utajiri ule wa chuma na makaa ya mawe katika maeneo ya Liganga na Mchuchuma, nikaona kuna suluhisho la matatizo yetu yanayoendelea kiuchumi.

Mchuchuma na Liganga

Madini ya chuma na makaa ya mawe ndiyo msingi wa maendeleo ya viwanda duniani kote. Nchi yetu ina madini haya yote kwenye eneo moja, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Katika eneo la Mchuchuma kuna mashapo yenye tani bilioni 1.2 za makaa ya mawe yenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 600 za umeme kwa miaka 150. Pia, makaa hayo hutumika kuyeyusha chuma na kuzalisha chuma cha pua. Vilevile eneo la Liganga lina mashapo ya madini ya chuma tani bilioni mbili ambayo ndani yake kuna madini yenye thamani kubwa ya titanium na vanadium.

Afrika nzima inajenga reli za kisasa na zote zinahitaji chuma kwa ajili ya kujenga njia za reli. Kenya na Ethiopia wamemaliza hatua za kwanza za reli zao; Kenya imeshajenga kilomita 485 kutoka Mombasa mpaka Nairobi na Ethiopia kilomita 760 kutoka Addis Ababa mpaka Djibouti.

Miradi yote hii mataruma ya reli yameagizwa kutoka nje na kuletwa Afrika, hivyo kuzalisha ajira huko kwenye nchi hizo (ambazo mataruma hayo yamezalishwa).

Tanzania ingeamua, ingeweza kulisha miradi yote ya reli chuma kutoka Ludewa katika nchi za (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa DRC) Kongo, Zambia, Angola, Uganda na Rwanda ambao wote wana miradi ya ujenzi wa reli na wamepanga kuagiza chuma kutoka China na kwingineko.

Bei ya tani moja ya chuma kwenye soko la dunia ni Dola 600 mpaka 1,000 za Marekani. Kwa hiyo Tanzania ikizalisha chuma tani milioni moja tu kwa mwaka, inaweza kupata mapato ya fedha za kigeni kati ya Dola 600 milioni mpaka bilioni moja kwa mwaka.

Jambo kubwa ambalo Tanzania imebahatika ni kwamba mashapo ya chuma yana madini mengine yenye thamani kubwa zaidi. Kwa mfano; vanadium ya Ludewa inauzwa tani moja kwa Dola 50,000 katika soko la dunia.

Katika kila tani milioni moja ya chuma kutoka Ludewa, kuna tani 80,000 ya vanadium. Tukiuza madini haya tunapata fedha za kigeni Dola 4 bilioni za Marekani kwa mwaka.

Ningefanya tofauti

Nchi yetu ina changamoto nyingi kiasi kwamba ni vigumu kuchagua ufanye ipi na uache ipi. Kiongozi mwenye maarifa huanza kutafuta fedha kwanza atekeleze majukumu mengine.

Viongozi wetu wa sasa wameamua kuanza kwa kutumia fedha za kodi au mikopo ghali yenye riba kubwa kutoka benki za biashara za nje.

Wameanza na ujenzi wa reli wa Dola 7 bilioni, ununuzi wa ndege wa zaidi ya Dola 1 bilioni (Dreamliner ‘Terrible Teen’) imenunuliwa kwa Dola 224 milioni na hata ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Rufiji maarufu Stiglers Gorge litakalogharimu Dola 3.5 bilioni.

Ningekuwa na mamlaka ningeyafanya haya yote, lakini kabla ya kufanya hayo, ningeanza kwanza kwa kufanya jambo moja kubwa ambalo lingenipa fedha za kufanya hayo. Ningefanya tofauti.

Ningeanza na mradi wa Mchuchuma na Liganga kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji unaanza mara moja na uzalishaji wa chuma na makaa ya mawe unafanyika bila kuchelewa. Ningehakikisha kuwa ndani ya miaka miwili tunaanza uzalishaji wa chuma, vanadium na titanium.

Mauzo ya vanadium peke yake ni sawa na Dola 4 bilioni nne kwa mwaka, kwa kuwa haya ni bidhaa ambatana na chuma maana yake asilimia 80 ya mapato haya yangekuwa ya nchi.

Kwa hiyo mwaka wa kwanza tu wa uzalishaji ningeweza kupata Dola 3.2 bilioni. Kwa fedha hizo, tungejenga reli kuanzia Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa mara moja bila kuungaunga na kubakia na chenji ya Dola 1 bilioni, ambazo ningeweza kujenga hospitali tano kubwa kama Mloganzila katika kanda tano za nchi; Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Arusha.

Ningeweza kujenga vyuo vya (ufundi stadi) Veta kila mamlaka ya serikali za mitaa nchini (wilaya, miji, manispaa na majiji) kwa kuwa unahitaji Sh750 bilioni tu kujenga vyuo hivyo vilivyokamili na vifaa vya kutosha vijana kupata mafunzo.

Ningeweza kujenga vyuo vikuu vipya vitatu aina ya (Chuo Kikuu cha Dodoma) Udom kwa kuwa Udom moja ina thamani ya Sh800 bilioni. Haya ni mapato ya mwaka wa kwanza tu. Kumbuka kuwa tunaweza kuendelea kuchimba chuma tani milioni moja kwa mwaka kwa miaka 2000.

Kwa nini hatuwekezi Mchuchuma na Liganga?

Kungoza nchi kunahitaji maarifa. Hakika ningefanya tofauti.