VIDEO-Polisi waeleza sababu za kumkamata Zitto

Muktasari:

Wakati polisi ikieleza hayo, baada ya kuachiwa Zitto ameeleza aliyoyakuta mahabusu jambo lililomlazimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei kutoa ufafanuzi.

Morogoro. Saa chache baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kuachiwa kwa dhamana, polisi imesema ilimkamata na kumuweka mahabusu kwa kuwa walifanya mkutano wa hadhara bila kuwa na kibali.

Wakati polisi ikieleza hayo, baada ya kuachiwa Zitto ameeleza aliyoyakuta mahabusu jambo lililomlazimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei kutoa ufafanuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 23, 2018 Kamanda Matei amesema Zitto alikamatwa jana, Februari 22 saa 11 jioni katika Kijiji cha Mhale, Wilaya ya Mvomero akiwa anafanya mkutano wa hadhara.

Kamanda Matei amesema Zitto anashtakiwa kwa kifungu 74 na 75 vya kanuni ya adhabu kwa kufanya mkutano bila kibali.

Kamanda huyo amesema awali Zitto alikuwa akifanya mkutano wa ndani, lakini baadaye wananchi walijaa nje na ndipo alipotoka kuwahutubia.

Zitto ameachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituo kikuu cha polisi cha mkoani Morogoro, Machi 12, 2018.

Hata hivyo, Zitto akizungumza na waandishi wa habari nje ya kituo cha polisi amesema yupo katika ziara ya kutembelea kata zinazoongozwa na madiwani wa chama hicho na kufanya vikao vya ndani.

Amesema ataendelea na ziara yake hiyo kama kawaida kwa kuwa kukutana ni haki ya kikatiba na hakuna mwenye uwezo wa kuizuia.

"Tunataka kuona wananchi wanapata haki zao za msingi bila kubughudhiwa na kukutana na kuzungumza ni haki ya msingi ya raia na hakuna mwenye uwezo wa kuinyang'anya," amesema Zitto.

"Sisi viongozi lazima tushuke chini kwa wananchi wetu ili kuona changamoto zinazowakabili na kwa pamoja tuzitafutie ufumbuzi.”

Amesema lengo la ziara yao ni kuzungumza na madiwani kuhusu utekelezaji wa ahadi zao kwa wananchi na kuangalia wamefanikiwa kuzitekeleza kwa kiasi gani.

Akizungumza alichokikuta mahabusu, amesema kuna watuhumiwa waliowekwa mahabusu muda mrefu bila kupelekwa mahakamani.

" Huko mahabusu nimekuta watuhumiwa zaidi ya 20  ambao wengi wao wamekaa mahabusu bila kufunguliwa mashataka yoyote. Inawezekana  Mungu ameamua niingie huko ili nijionee mateso wanayopata,” amesema.

Hata hivyo,  Kamanda Matei amekanusha madai ya uwepo wa watuhumiwa wa muda mrefu katika kituo hicho akidai wote hufikishwa mahakamani kwa wakati.