Zitto ahoji ubora wa ‘Ndege ya Magufuli’ bungeni

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akizugumza vikao vya Bunge, mjini Dodoma hivi karibuni. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Hiyo ni moja kati ya ndege ambazo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imepanga kuzinunua katika mkakati wake wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Tayari imeshanunua mbili aina ya Bombardier.

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amehoji viwango vya ndege inayonunuliwa na Serikali aina ya Dreamliner akisema ndege hizo zilikataliwa na mashirika mengine ya dunia kutokana na ubora wake.

Hiyo ni moja kati ya ndege ambazo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imepanga kuzinunua katika mkakati wake wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Tayari imeshanunua mbili aina ya Bombardier.

Zitto alisema hayo katika mchango wake wa maandishi kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juzi usiku. Mjadala huo wa siku tatu utaendelea Jumanne ijayo ambapo Waziri Makame Mbarawa atajibu hoja za wabunge.

“Ndege hizi zinaitwa ‘Terrible Teens Dreamliners’ ambazo zilikuwa 12 na zilikosa soko kwa sababu ni nzito na hazina viwango,” alisema.

Alisema pia Ethiopia imenunua ndege hizo lakini kwa punguzo kubwa la bei kwa sababu hazikuwa na soko.

“Wajibu wangu kama mbunge ni kuisimamia Serikali na kuhakikisha fedha za Watanzania zinatumika kwa uwazi na kwa umakini. Hivyo naomba maelezo ya Serikali kuhusu suala hili ili Watanzania wajue kama fedha zao zinatumika vizuri,” alisema.

Alisema mwaka jana, Serikali ilitenga Sh500 bilioni kununua ndege na mwaka huu pia kiasi kama hicho na tayari imelipa asilimia 30 ya dola za Marekani 224 milioni kununua Dreamliner.

Zitto alisema kwa miaka miwili, zimetumika Sh1 trilioni ambazo ni alisema ni uamuzi mgumu wakati hakuna chakula katika Ghala la Taifa na watoto wanakosa mikopo ya elimu ya juu kwa sababu tunanunua ndege.

“Bajeti ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima wetu imepungua kutoka Sh78 bilioni mpaka Sh10 bilioni kwa sababu tunanunua ndege, fedha ya vifaa tiba na dawa hospitalini ni ndogo kwa sababu tunanunua ndege. Ni maamuzi. Kupanga ni kuchagua,” alisema.

Akizungumzia ndege hizo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige alisema fedha zilizotengwa mwaka jana na mwaka huu kununua ndege hizo ni uwekezaji makubwa na kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema umakini unahitajika katika kuiendesha ATCL hivyo Serikali isiishie tu kulipatia ndege, kwa kuwa linahitaji mtaji wa uendeshaji na rasilimali watu ili liweze kujiendesha kibiashara.

Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alimtaka waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa awapuunze wanaobeza miradi mikubwa inayofanywa na Serikali kwa kuwa hiyo ni ishara kuwa anafanya vizuri.

“Ukiona adui yako anakupongeza kwa jambo fulani unalofanya hilo achana nalo, lakini ukiona anakupinga hilo endelea nalo maana utakuwa unafanya vizuri,” alisema.

Alisema waziri huyo amevaa kiatu cha Rais Magufuli aliyekuwa waziri wa ujenzi kabla yake na kimemwenea.