Zitto aichambua Bajeti ya Serikali

Kiongozi wa Chama cha Act-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano  kuhusu uchambuzi wa bajeti ya mwaka 2018/19 uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Juzi, kambi hiyo inayoundwa na muungano wa Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF ilitaja vipaumbele vitano ambavyo itavisoma leo, bungeni jijini Dodoma. Vipaumbele vya bajeti mbadala ni elimu; kilimo, mifugo na uvuvi; viwanda vya mazao ya kilimo; afya na maji, pamoja na utawala bora.

Dar es Salaam. Baada ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuichambua bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19, jana ilikuwa zamu ya Chama cha ACT Wazalendo ambayo imetaja maeneo yanayostahili kuwekewa msisitizo.

Juzi, kambi hiyo inayoundwa na muungano wa Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF ilitaja vipaumbele vitano ambavyo itavisoma leo, bungeni jijini Dodoma. Vipaumbele vya bajeti mbadala ni elimu; kilimo, mifugo na uvuvi; viwanda vya mazao ya kilimo; afya na maji, pamoja na utawala bora.

Mbali ya ACT Wazalendo, wadau wengine waliotoa uchambuzi wao jana ni wazalishaji wa vinywaji vikali nchini pamoja na mtandao wa asasi za kiraia wa Policy Forum.

Kama ilivyosema kambi rasmi ya upinzani, ACT Wazalendo nayo imesema zipo changamoto kwenye utekelezaji wa bajeti hiyo na kutoa ushauri juu ya masuala kadhaa yanayohitaji kufanyiwa kazi.

Akiwasilisha uchambuzi huo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema Serikali inapaswa kuzizingatia sekta zinazowagusa zaidi wananchi na kuzipa kipaumbele.

“ACT inapendekeza vipaumbele vinne ambavyo ni kuimarishwa kwa kilimo, viwanda, huduma za jamii kama vile maji, na ujenzi wa miundombinu wezeshi hususan ya nishati na usafirishaji,” alisema Zitto.

Alisema hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wiki iliyopita inataja marekebisho ya kikodi yanayolenga kukuza sekta ya viwanda, utalii, kukuza ajira na kuongeza mapato lakini kilimo na huduma za jamii havijatajwa jinsi vitakavyotekelezwa.

Kutokana na hilo, chama hicho kimependekeza mambo matano kuisaidia Serikali kutekeleza bajeti hiyo licha ya changamoto zilizopo.

Kwanza, imependekeza kutungwa kwa mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka kwa sekta ya kilimo ili kumuwezesha mkulima kubaki na sehemu kubwa ya mapato na kuwavutia wananchi wengi zaidi kuwekeza huko.

Pia, kimeishauri Serikali kuharakisha kuanzishwa kwa soko la bidhaa ili kupunguza watu wa kati katika sekta ya kilimo na kuanzisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wakulima kwa kuanzisha mafao ya bei ili kuhakikisha gharama zao pindi bei zinapotetereka zinarudi.

“Serikali ifanye uamuzi wa kisera kuhakikisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi vinapewa vivutio vya kikodi,” alishauri Zitto.

Alishauri kuwapo kwa utaratibu rahisi wa kuanzisha viwanda na kuweka mfumo wa kisheria kufidia baadhi ya gharama za uzalishaji kwa bidhaa zinazozalishwa na wananchi wengi kama vile saruji, mafuta ya kula na sukari.

Angalizo

Zitto alisema utekelezaji wa bajeti ijayo utakuwa mgumu kutokana na kutowezekana kukusanywa mapato yote ya ndani yanayotarajiwa. Alisema kwenye bajeti iliyosomwa, Serikali inakusudia kukusanya Sh23.6 trilioni kutoka vyanzo vya ndani lakini, alikumbusha kuwa mwenendo unaonyesha unaonyesha kuwapo kwa nakisi kwenye uhalisia.

Alisema kwa miaka mitatu ya mwisho ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, nakisi hiyo ilikuwa wastani wa asilimia sita lakini sasa wastani huo umeongezeka mpaka asilimia 14.

Kwa kuwa sekta ya maji na kilimo zinawagusa wananchi wengi zaidi nchini, ACT Wazalendo imeshauri kuanzishwa kwa ushuru maalumu kuziwezesha wizara husika ikiwa ni mkakati wa kuongeza mapato.

Chama hicho kimetaka uanzishwe ushuru wa Sh160 kwenye mafuta na Sh100 zipelekwe kwenye mfuko wa maji na Sh60 kwenye mfuko wa umwagiliaji, “Ushuru huu utasaidia kuongeza Sh366 bilioni kwenye wizara hizo,” alibainisha.

Kabla ya kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) mwaka 2016, alisema sekta ya utalii ilikuwa inakua kwa asilimia 12 lakini baada ya hapo ukuaji wake ni asilimia tatu tu hivyo alishauri iondolewe ili sekta hiyo ikue kwa wastani wa tarakimu mbili na kuongeza mchango wake kwenye mapato ya Serikali.

Kwenye viwanda ambako Serikali imetangaza kuondoa Vat kwenye taulo za kike na kupunguza kodi ya kampuni kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano, chama hicho kimeshauri kusamehewa pia kwa ushuru wa bidhaa na kodi ya mapato.

“Tatizo si kodi, changamoto kubwa ya sekta ya ngozi ni magendo. Serikali izuie uuzaji wa ngozi ghafi na kuanzisha ruzuku kwa watakaoongeza thamani ya bidhaa hizo,” alishauri Zitto akitoa mfano Ethiopia ambako tani moja ya ngozi iliyosindikwa hulipwa Dola 30 za Marekani.

Tangu kuanzishwa kwa Vat kwenye miamala wa simu Julai mwaka jana, Zitto alisema kiasi cha miamala kimepungua kwenye sekta ya mawasiliano hivyo kuishauri Serikali kuufuta ushuru huo wa asilimia 10.

ACT Wazalendo imependekeza kupunguzwa kwa michango ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka asilimia 20 mpaka 12 ambazo wafanyakazi watachangia asilimia tano na waajiri asilimia saba na tozo ya kuendeleza ujuzi (SDL) ishushwe mpaka asilimia mbili.

Kuheshimu bajeti

Ili kuhakikisha kunakuwa na ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi yaliyokusudiwa na kuidhinishwa na Bunge, Zitto alisema kunahitaji nidhamu kubwa ya Serikali na watendaji wake.

Kutokana na vyanzo vilivyopo, alikumbusha kuwa ukusanyaji umekuwa haufikii lengo liliokusudiwa kwa muda mrefu huku kukiwa na changamoto ya kubadili vipaumbele katikati ya utekelezaji wa bajeti hiyo.

Alisema uuzaji wa mazao ya kilimo, madini na bidhaa za viwandani umepungua kwa kiasi kikubwa jambo litakaloongeza ugumu wa kukusanya mapato ya kutosha hivyo kutahadharisha kuhusu matumizi ambayo hayakupitishwa.

“Ufanisi wa sekta nyingi umeshuka. Usafirishaji wa pamba, korosho, kahawa madini kama almasi umeshuka. Tusipoheshimu bajeti iliyopitishwa, itakuwa ngumu kufanikisha malengo yaliyopo,” alisema.

Licha ya kuheshimu bajeti, alishauri mipango mizuri inayopitishwa itekelezwe kwa ukamilifu ili kuondoa hali ngumu kwa wakulima na wafanyakazi.

Kwenye mfumo wa stempu za kieketroniki, alisema upo uwezekano mkubwa wa kupanda kwa ushuru wa bidhaa hivyo kuongezeka kwa bei kutakakowaumiza wananchi.

“Kwa kuwa umma haukujulishwa kuhusu zabuni ya mkandarasi huyu, basi itangazwe zabuni ya wazi ya kimataifa ili kushindanisha bei au Serikali iwekeze yenyewe kwenye mfumo huo,” alishauri.

Kodi ya wafanyakazi

Zitto alisema kwa kuzingatia kuwa mfumuko wa bei na mishahara ya watumishi kutoongezwa kwa miaka mitatu sasa, ipo haja ya kubadilisha viwango vya kodi.

Mapendekezo ya chama hicho ni kwamba wafanyakazi wanaolipwa chini ya Sh360,000 wasitozwe kodi yoyote, bali wanaozidi kiasi hicho ndio walipe PAYE. Licha ya kima cha chini, chama hicho kimependekeza kodi inayolipwa na wenye mishahara ya juu, zaidi ya Sh15 milioni kwa mwezi.