VIDEO-Zitto ataja mambo 12 yanayowakera wananchi

Muktasari:

  • Alisema hayo baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea kata zinazoongozwa na ACT-Wazalendo nchini, iliyoanza Februari 13.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametaja mambo 12 aliyobaini kuwa ni changamoto kwa wananchi wa vijijini ukiwamo ufukara na akapendekeza Serikali kujikita zaidi katika maendeleo ya watu badala ya miradi mikubwa.

Alisema hayo baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea kata zinazoongozwa na ACT-Wazalendo nchini, iliyoanza Februari 13.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, Zitto alisema hali ya maisha aliyoikuta katika vijiji vya kata alizozitembelea ni ya ufukara.

Akikariri utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa) na Afrobarometer, alisema asilimia 76 ya Watanzania wana ufukara wa kipato sasa ikilinganishwa na asilimia 64 ya mwaka 2014, “Hawa hawana uwezo wa kununua, kulipia huduma za afya, kununua mbegu bora, mbolea na mlo bora.”

Alisema jambo muhimu ni wananchi kupata mahitaji muhimu ndipo miradi ya vitu ifuate.

“Ujenzi wa reli utakuwa na maana kubwa kama wananchi watakuwa wanapata mahitaji muhimu ya kijamii,” alisema.

Kuhusu njaa, Zitto alisema kwa mujibu wa utafiti wa Repoa, asilimia 27 ya Watanzania wanalala na njaa sasa kulinganisha na chini ya robo ya Watanzania waliolala njaa mwaka 2014.

“Hali ya watu kula mlo mmoja badala milo mitatu katika vijiji tulivyotembelea limekuwa jambo wanalolizoea sasa,” alisema.

Masuala mengine aliyoyazungumzia ni udumavu, vifo vya wazazi, ukosefu wa ajira, changamoto ya ardhi na tatizo la maji vijijini.

Juhudi za Mwananchi kuwapata mawaziri wa Kilimo, Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi kuzungumzia madai hayo ya Zitto ziliogonga mwamba jana baada ya simu zao kuita bila kupokewa au kutopatikana.

Hata hivyo, Januari 8, Dk Abbasi alitaja mambo saba yanayoonyesha mafaniko ya utekelezaji wa ahadi za Serikali ambayo pia yanagusia hoja za Zitto akisema miongoni mwa mafanikio hayo ni kuendelea kukua kwa uchumi kiasi cha kuziridhisha taasisi mbalimbali za kimataifa, utekelezaji wa ahadi ya kuhamia Dodoma, ununuzi wa meli, miradi ya umeme, zabuni ya ununuzi wa injini na mabehewa ya treni ya kisasa na kuendelea kujengwa kwa uchumi wa viwanda.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano bora za Afrika ambazo uchumi wake unakua na kuimarika, kwamba ina viwanda 3,330 vilivyosajiliwa, kati ya hivyo 652 ni vikubwa na 2,700 vidogovidogo.

Mambo mengine

Zitto alisema mambo mengine aliyojionea katika ziara hiyo ni viwanda kufungwa au kusitisha uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi na hivyo kusababisha gharama ya bidhaa kupanda.

Kuhusu mbolea, Zitto alidai kwamba bei ya mbolea imepanda kutoka kati ya Sh41,000 na Sh54,000 kwa mfuko wa kilo 50 mpaka kufikia kati ya Sh47,000 na Sh57,000.

Alisema masuala mengine ni migogoro ya ardhi kati ya watumiaji wadogo na wawekezaji wakubwa.

Alisema kiini cha migogoro hiyo ni ukiukwaji wa sheria unaofanywa na watendaji wa Serikali wenye dhamana ya kutekeleza sheria.

Hatua zilizochukuliwa

Kiongozi huyo alisema atapeleka bungeni mpango mbadala wa kupinga mpango wa sasa wa bajeti unaojikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya watu.

Alisema masuala watakayoyasimamia ni uchumi shirikishi unaozalisha ajira kwa kuhakikisha kilimo na viwanda ndiyo vipaumbele.

Kuhusu ardhi, alisema wamemwandikia, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ili aingilie suala hilo.

Alisema uhifadhi umekuwa ukiingilia ardhi ya vijiji na kuchukua maeneo makubwa na kusababisha adha kubwa kwa wananchi.

Akijibu madai hayo, waziri Lukuvi alisema bado hajapokea barua kutoka kwa Zitto kuhusiana na changamoto hizo katika maeneo alikofanya ziara.
“Serikali ya Awamu ya Tano haina ubaguzi wa vyama vya siasa, tunatatua changamoto za wananchi kwa kufuata sheria zilizopo, alete hiyo barua mimi bado sijaipata,” alisema Lukuvi

Kuhusu afya na elimu, mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema ACT - Wazalendo itashiriki katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, madarasa na nyumba za walimu kwenye kata inazoziongoza.

“Ili kukabiliana na hali tuliyoikuta kwenye kata tunazoziongoza, chama kinafanya tathmini ya kujua mahitaji na itahamasisha wanachama kuchangia gharama za ujenzi,” alisema.

Mapendekezo kwa Serikali

Zitto alisema chama hicho kimependekeza mambo kadhaa, ikiwamo kuzitaka taasisi za utafiti kama Repoa kufanya utafiti kuhusu rasilimali za kibajeti zinavyogawanywa kati ya mijini na vijini.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya wananchi wa vijijini ni mabaya mno ikilinganishwa na mijini,” alisema.

Alisema miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha iko kwenye miji mikubwa na kwamba mfumo unaoendelea unawanyonya watu wa vijijini.

Alisema taasisi hizo zifanye uchambuzi na matokeo yawekwe kwa umma ili kupata namna nzuri ya mgawanyo wenye tija wa mapato kati ya vijijini na mijini.

Alisema Serikali imeainisha vipaumbele vya kibajeti kwa mwaka 2018/19.

“Lakini masuala ya watu kama kilimo na maji hayamo kwenye vipaumbele, hivyo rai yetu ni kwamba Serikali ijitazame katika eneo hilo,” alisema.

Kuhusu demokrasia, Zitto aliendelea kusisitiza kuitishwa kwa mkutano wa kitaifa wa maridhiano ya kisiasa ili kuzijadili changamoto za uendeshaji wa siasa nchini.

Kuhusu usalama wa nchi, chama hicho kimependekeza kuundwa kwa tume huru kuchunguza matukio ya mauaji, utekwaji nyara na kupotea kwa watu.

Kuhusu uwajibikaji, alisema wizara ya Tamisemi ihakikishe kuwa halmashauri zinazoongozwa na CCM zinatekeleza maelekezo ya kamati ya fedha na uongozi iwe angalau na diwani mmoja wa chama cha upinzani.

“Ziara yetu imeonyesha halmashauri nyingi zinazoongozwa na CCM hazifuati agizo hilo na hivyo kuondoa kabisa nafasi ya uwajibikaji na usimamizi wa mapato ya halmashauri,” alisema.

ACT yafungua kesi

Aidha, Zitto alisema chama hicho kimefungua kesi ya madai namba 8 ya mwaka 2018 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kulishtaki Jeshi la Polisi kwa kuingilia isivyo halali shughuli za chama hicho.

Februari 23, Zitto aliwekwa mahabusu na Polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa akifanya mkusanyiko bila kibali katika Kata ya Kikeo, Mvomero na alihojiwa katika kituo cha Polisi Dakawa na kuhamishiwa Morogoro Mjini.

Zitto alifanya ziara ya kuitembelea mikoa minane yenye kata zinazoongozwa na ACT - Wazalendo ili kuwashukuru kwa kuwachagua wawakilishi wa chama hicho, kushiriki kazi za maendeleo na kuzungumza na kamati za maendeleo za kata hizo.