Zitto ataka tafakuri ya Mbowe isilenge kubagua watu

Muktasari:

Zitto pia ameeleza jinsi umoja huo utakavyokuwa na malengo yake, akisema si wa vyama pekee bali makundi yote katika jamii dhidi ya utawala usiofuata demokrasia nchini.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutaka tafakuri pana kuhusu kuundwa kwa umoja wa demokrasia nchini, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameshauri isilenge kubagua watu.

Zitto pia ameeleza jinsi umoja huo utakavyokuwa na malengo yake, akisema si wa vyama pekee bali makundi yote katika jamii dhidi ya utawala usiofuata demokrasia nchini.

Awali katika mazishi ya Kasuku Bilago aliyekuwa mbunge wa Buyungu (Chadema) yaliyofanyika katika Kijiji cha Kasuga wilayani Kakonko, Zitto na Mbowe walizungumzia kuweka mgombea mmoja wa jimbo hilo.

Siku iliyofuata, Mbowe alisema suala la kuunda umoja utakaovishirikisha vyama vya upinzani nchi nzima linahitaji tafakuri ya kina, ikiwa ni pamoja na kushirikisha vikao vya chama.

Zitto alipotafutwa na Mwananchi jana kuzungumzia kauli ya Mbowe, alisema amezingatia wazo la kiongozi huyo wa Chadema lakini tafakuri isiwe ya kubagua watu.

“Muhimu tusibague watu. Wakati huu ni wa kuimarisha nguvu kulinda demokrasia ya vyama vingi nchini. Muhimu ni kuweka vigezo na washirika kuzingatia vigezo. Tunahitaji united democratic alliance (ushirikiano wa kidemokrasia) kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Zitto.

“United Democratic Front ni movement inayohusisha makundi ya jamii zaidi ya vyama vya siasa.”

Zitto alisema wazo la kuanzisha umoja huo limetokana na maazimio ya kikao cha kamati kuu ya ACT Wazalendo.

“Chama cha ACT Wazalendo katika kikao chake cha kamati kuu cha Januari, kiliazimia katika mwelekeo wa chama mwaka 2018 kuwa ni muhimu kujenga ushirikiano na vyama na makundi mengine ya kijamii,” alisema Zitto.

“Mwelekeo huo, tunataka kujenga democratic front kwa kuhusisha wana demokrasia nchini kwa madhumuni ya kwanza kutetea, kuimarisha na kulinda demokrasia yetu ya vyama vingi. Pili, kujenga uchumi shirikishi wa wananchi.”

Kuhusu mwelekeo wa ACT Wazalendo, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini alisema ni pamoja na kupigania haki za wafanyakazi kupitia vyama vyao na haki za raia kupitia vyama vya wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara wadogo kwa kujenga ushirikiano na jumuiya hizo za wananchi. “Kuongoza juhudi za ushirikiano na vyama vingine vya upinzani kwa shabaha ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini, kwa kufanya vikao vya mara kwa mara na viongozi wa vyama vingine na kufanya shughuli za pamoja,” alisema.

Aliongeza kuwa mambo mengine ni kuendelea kusemea haki za kijamii kama elimu na afya na kuongeza juhudi za kupigania haki ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wote hasa wakulima kwa kushawishi kuanzisha fao la bei katika mfumo wa hifadhi ya jamii na bima ya afya kwa kila Mtanzania.

Alitaja mwelekeo mwingine kuwa ni kuendelea kushawishi sera za uchumi zinazomkomboa mwananchi wa kawaida kwa kukosoa sera zinazodidimiza maendeleo ya uchumi na kupendekeza sera mbadala.

Licha ya kutotaja walengwa, Zitto alisema tayari chama chake kimeshaanza mazungumzo na vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyama vya wafanyakazi ili kufikia azma hiyo. “Sisi kama chama tumeanza vikao vikiwamo na vyama vya siasa na asasi za wananchi kama vyama vya wafanyakazi na vikundi vya wakulima. Pia, tunajadiliana na NGOs,” alisema.

Alisema lengo ni kuunganisha watu na taasisi zote zinazotaka kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini na kulinda demokrasia ya vyama vingi.

Alisema wameshamaliza vikao na hatua inayofuata ni kuanza majadiliano na vyama na asasi ili kuhalalisha muungano huo