Zitto atilia shaka Akiba ya Taifa, Gavana amtoa hofu

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

Wasiwasi wa Zitto umetokana na taarifa ya mwenendo wa uchumi iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Julai 20, inayoonyesha kuwa akiba iliyopo nchini inaweza kuagiza bidhaa zitakazotumika kwa miezi 3.6 tofauti na iliyokuwapo Novemba mwaka jana ambayo ingetosha kwa miezi 4.1.

Dar es Salaam. Wakati Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akieleza wasiwasi wake kuhusu kupungua kwa Akiba ya Taifa ya fedha za kigeni, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndullu amesema bado ipo akiba ya kutosha.

Wasiwasi wa Zitto umetokana na taarifa ya mwenendo wa uchumi iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Julai 20, inayoonyesha kuwa akiba iliyopo nchini inaweza kuagiza bidhaa zitakazotumika kwa miezi 3.6 tofauti na iliyokuwapo Novemba mwaka jana ambayo ingetosha kwa miezi 4.1.

“Kuna jambo kubwa linaendelea kwenye akiba ya fedha za kigeni ya Tanzania. Ama Serikali kupitia Benki Kuu inapunguza akiba ili kuibeba shilingi isishuke thamani au akiba imetumika kwa matumizi ya kawaida. Serikali haina budi kutoa maelezo ya kina,” alisema Zitto.

Kauli ya kiongozi huyo wa upinzani imetokana na kumbukumbu za BoT zilizokuwapo Novemba mwaka jana ambazo zinabainisha, Tanzania ilikuwa na Dola za Marekani bilioni nne ambazo zingetosha kuagiza bidhaa kwa miezi minne.

Akiba hiyo iliendelea kupungua kwani mpaka Machi, kulikuwa na Dola 3.8 bilioni na Juni zikawa Dola 3.5 bilioni.

“Katika kipindi ambacho bei ya mafuta duniani ipo chini na mauzo ya nje bado hayajashuka, ilitakiwa akiba yetu iongezeke siyo kupungua,” alisema Zitto.

Alisema Taifa kuwa na akiba isiyoweza kuhudumia kwa miezi sita ni jambo la hatari ambalo wachumi na watunga sera hawana budi kuliangalia kwa jicho la ziada kabla uchumi haujaathirika kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, Profesa Ndullu alisema kupungua kwa takwimu hizo kunatokana na njia iliyotumika kukokotoa.

“Sisi tunatumia akiba ghafi wakati IMF wanapendelea ile halisi. Tofauti imepatikana hapo,” alisema Gavana huyo.

Alisema kwa takwimu zilizopo BoT, akiba iliyopo inatosha kutumika kwa miezi minne na zaidi na kwamba kiasi hicho kimekuwapo mwaka jana.

“Uagizaji wa bidhaa kutoka nje umepungua kwa Dola 2.9 bilioni, hasa mafuta. Hii nayo ni sababu muhimu unapozungumzia Akiba ya Taifa,” alisema Profesa Ndullu.

Pamoja na hoja hiyo, katika ripoti yake, IMF imeeleza juu ya kukua kwa uchumi na kuimarika kwa sekta za ujenzi, uchukuzi, mawasiliano na fedha. Kupungua kwa deni la ndani pia ni suala lililoelezwa kuimarisha uchumi kwa ujumla.

“Wakurugenzi wameridhishwa na hatua za Serikali kuimarisha vyanzo na usimamizi wa kodi,” inasomeka taarifa hiyo.

Mwanazuoni wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe alisema kiasi kilichoshuka hakitishi, ndiyo maana hata IMF hawajaonya juu ya suala hilo.

“Hiki ni kiwango ambacho Taifa linaona kinafaa kuwapo ili kitumike pindi mambo yatakapokuwa magumu. Tofauti ni ndogo kutokuwa na madhara,” alisema Profesa Wangwe.