Zitto atoboa alichozungumza na Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe  

Muktasari:

Wawili hao walikutana ofisini kwa waziri huyo wa zamani kujadili masuala mbalimbali na hasa mwenendo wa kisiasa nchini.

 


Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hali ninayoendelea kwenye uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani ni ishara ya kitakachojiri mwaka 2020 na kutaka wadau wa demokrasia kuungana kuitetea.

Amesema hayo muda mfupi baada ya ofisi ya WaziriMkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali wa zamani, alikuwa na mazungumzo na Zitto leo asubuhi Julai 19,2018.

Katika kufuatilia taarifa hiyo ya ofisi ya Lowassa iliyoambatana na picha inayowaonyesha wawili hao wakiwa wanatabasamu, Mwananchi Digital ilithibitishiwa na Zitto kuwepo kwa mazungumzo hayo.

Na kama taarifa ya ya ofisi ya Lowassa iliyotumwa na msaidizi wake, Aboubakar Liongo ilivyoeleza, Zitto na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema walizungumzia mwenendo wa siasa nchini.

“Udanganyifu unaotokea katika chaguzi hizi unatia wasiwasi na ni ishara za wazi za hali tutakayokutana nayo mwaka 2020 (wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao),” ameandika Zitto katika ujumbe wa simu kwa Mwananchi.

“Kama wapinzani na wadau wengine wa demokrasia, huu ni wakati wa kuunda umoja imara kupinga uondoaji wa demokrasia yetu na kuzuia kasi ya kukua kwa utawala wa amri. Tayari chama chetu kinafanya mazungumzo na vyama vingine.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Liongo mazungumzo ya wawili hao yaliyofanyika ofisini kwa Lowassa, yalihusu mwenendo wa hali ya siasa nchini na mchango wa vyama vya siasa kwenye maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kwa undani kilichozungumzwa.

Hivi sasa, mchakato wa uchaguzi mdogo katika kata 77 na jimbo moja unaendelea na tayari CCM imeshapata madiwani 20 waliopita bila ya kupingwa baada ya kuwekewa upinzani na wagombea wa CCM au wasimamizi kuwaengua kwa madai ya kukosa sifa.

Wapo walioondolewa kwa kutoandika kwa usahihi neno “zinjathropus”, wako walioenguliwa kwa sababu walituhumiwa kwa mauaji, huku waengine wakienguliwa kwa madai ya kudai kazi zao ni wakulima wakati ni wa wafanyabiashara.

Wako pia walioenguliwa kwa madai kuwa si raia na walioenguliwa kwa madai ya kutoa namba ya simu ambazo wasimamizi walidai si sahihi.

Maamuzi hayo yameibua rufaa kutoka Chadema ambayo imesema wasimamizi wamekiuka sheria na taratibu za uchaguzi.