Zitto aupokea uamuzi wa Serikali kununua korosho lakini...

Muktasari:

  • Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameunga mkono hatua iliyochukuliwa na Serikali kununua korosho zote za wakulima katika msimu huu kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo akidai huo ni msimamo wa chama chake.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ameupokea uamuzi wa Serikali kununua korosho yote ya wakulima lakini Serikali itakosa mapato.

Zitto amedai sababu za kushuka kwa uzalishaji wa korosho katika msimu wa mwaka 2018 ni hatua ya Serikali kupora fedha za wakulima.

Taarifa ya ACT- Wazalendo iliyotolewa na Zitto leo imeleza kuukaribisha uamuzi huo wa Serikali huku chama hiho kikidai huo ndiyo ulikuwa msimamo wake tangu awali.

“Chama cha ACT- Wazalendo tunakaribisha uamuzi wa Serikali kununua kwa bei nzuri korosho zote za wakulima wa korosho kama tulivyopendekeza,” amesema Zitto kwenye taarifa hiyo huku akirejea mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika Oktoba 28.

Amesema kwenye mkutano huo chama chake kilitoa mapendekezo kwamba Serikali inunue Korosho zote za wakulima ili kuwalinda na bei ndogo kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo kwenye soko la dunia.

“Kwa vile malengo ya Serikali hayatakuwa kupata faida bali kufidia gharama za manunuzi, bei ya korosho haitashuka sana. Kisha Serikali iwauzie wanunuzi kwa namna wanaona inafaa. Lengo hapa ni kumlinda Mkulima kwa kumpa bei nzuri,” amesema.

Hata hivyo, Zitto ameinyooshea kidole Serikali kwa kusema kushuka kwa uzalishaji mwaka huu kunatokana na Serikali kupora fedha za wakulima wa korosho.

Amesema uzalishaji wa korosho kwa msimu wa 2018 unatarajiwa kushuka kwa asilimia 43 kutoka tani 350,000 mwaka 2017 mpaka tani 200,000 mwaka huu.

Zitto amesema licha ya Serikali kutoa sababu ya hali ya hewa kama sababu ya uzalishaji kupungua, sababu kubwa ni wakulima kukosa pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu kutokana na fedha zao kuporwa na Serikali.

Pamoja na hatua nzuri iliyochukuliwa, Zitto amesema Serikali itakosa mapato ya fedha za kigeni ambayo ni muhimu katika kutunza thamani ya sarafu ya nchi.

Amesema Watanzania watakaoathirika kwenye mnyororo wa thamani ni wenye magari ya usafirishaji, wamiliki wa nyumba za wageni, wenye migahawa, makuli, mawakala wa meli pamoja na wamiliki wa maghala.

“Pia, Serikali itakosa mapato ya kodi (Export Levy) pamoja na mapato ya kodi ya halmashauri za miji inayolima korosho. Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba itaathirika zaidi kwani ilitarajia kupata Sh5 bilioni mwaka huu,” amesema Zitto.