Zomeazomea yaibuka bungeni, wabunge wapingana ushuru wa korosho

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akiwatuliza wabunge kambi ya upinzani waliokuwa wakizomea wakati wabunge wakijadili mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu awaonya asema asiyeweza kuvumilia mchango wa mwenzake atoke nje ya ukumbi wa Bunge


Dodoma. Zomeazomea imeibuka katika ukumbi wa Bunge leo Jumatatu Juni 25, 2018 na kumfanya mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuwaonya wabunge wanaofanya vitendo hivyo, akiwataka wanaoshindwa kuheshimu michango ya wenzao kutoka nje.

Jambo hilo limetokea wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19 baada ya kuibuka mvutano wa pande mbili bungeni.

Mvutano huo unawahusu wabunge wanaoitetea  Serikali kutotoa asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo na wanaopinga jambo hilo pamoja na mabadiliko ya Sheria ya Korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

Zomezomea hiyo iliibuka baada ya mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Ngonyani kuunga mkono hoja ya Serikali ya kuchukua asilimia zote 100 za ushuru wa mauzo ya korosho nje.

“Ushuru wa mauzo ya korosho umekuwa ukipotoshwa sana. Waziri Mkuu anatoka nyanda za juu kusini asingekubali kuweka utaratibu mbovu. Suala hili wanatozwa wafanyabishara wakubwa na haitozwi kwa wakulima,” amesema mbunge huyo.

“Naunga mkono hii hoja ya asilimia 35 na asilimia 65 zipelekwe mfuko wa Serikali.”

Kauli hiyo ilimnyanyua mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara maarufu Bwege, “huyu anayesema sasa hivi (Ngonyani) kuwa mfuko wa Hazina utatunza vizuri hizi fedha  kabla ya kusema hivyo tuleteeni fedha zetu za Korosho.”

Akiendelea kuchangia katika mjadala huo, Jacqueline amesema, “ni vizuri fedha hii ikapelekwa katika mfuko mkubwa ili fedha hizi tuzifaidi nchi nzima. Ngariba yoyote haogopi mkojo.”

Akitolea ufafanuzi mvutano huo, Zungu amewataka wabunge kuheshimu michango ya wenzao.

“Kama hampendi anachozungumza  tokeni nje mkakae canteen (kwenye mgahawa). Natoa onyo la mwisho, wote mnaozomea nawaona naomba mkae kimya. Majibu ya Serikali yatatolewa na kama hupendi kaa kimya na kama hutaki kukaa kimya nitakutoa nje,” amesema Zungu.