Zuio usafirishaji makinikia laipa hasara Acacia

Muktasari:

  • Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kupata hasara tangu mabadiliko ya Sheria ya Madini ilipofanywa mwaka jana kuipa Serikali fursa ya kunufaika zaidi na rasilimali za Taifa.

Dar es Salaam. Kutokana na zuio la usafirishaji wa makinikia lililowekwa tangu Machi mwaka jana, kampuni ya Acacia imepata hasara ya Dola 19.1 milioni (zaidi ya Sh43 bilioni) katika robo ya pili ya mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kupata hasara tangu mabadiliko ya Sheria ya Madini ilipofanywa mwaka jana kuipa Serikali fursa ya kunufaika zaidi na rasilimali za Taifa.

Ofisa mtendaji mkuu wa Acacia, Peter Geleta alisema kwa robo ya kwanza, kampuni hiyo ilikuwa na ufanisi katika uzalishaji baada ya kuchimba wakia 254,759 kwa gharama himilivu.

“Kwa miezi sita ya kwanza malengo yetu yalikuwa kupunguza gharama za uendeshaji kuendana na sintofahamu iliyopo kutokana na mgogoro uliopo baina yetu na Serikali. Tutaendelea kuchukua hatua kukidhi mahitaji ya wadau,” alisema Geleta.

Alisema mabadiliko waliyofanya mwishoni mwa mwaka jana yalichangia kupata mafanikio katika miezi mitatu ya kwanza, hivyo wanatarajia kuzalisha kati ya wakia 435,000 na 475,000 mwaka huu.

Kutokana na uzalishaji imara kwenye robo ya kwanza mwaka huu, kampuni hiyo ilipata faida ya Dola 35.7 milioni (zaidi ya Sh80 bilioni) ambazo taarifa ya hesabu za fedha kwa nusu iliyoishia Juni inaonyesha imeshuka mpaka hasara ya Dola 19.1 milioni katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni. Katika miezi hiyo mitatu, Acacia ilizalisha wakia 133,778 zilizoshuka kutoka 254,759 zilizozalishwa kati ya Januari na Machi, hivyo kushusha mapato kutoka Dola 333.3 milioni mpaka Dola 176.9 milioni.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa kushuka kwa uzalishaji kunachangiwa na zuio la usafirishaji wa makinikia kwa asilimia 36, hivyo menejimenti kupendekeza kutolipwa kwa gawio katika robo hiyo.

Hayo yakitokea, kampuni mama ya Acacia, Barrick Gold Mine inaendelea kufanya mazungumzo na Serikali kutafuta muafaka kuhusu faini ya kodi na malimbikizo yake yanayofika Dola 190 bilioni na kupata hatima ya usafirishaji wa mchanga huo wa madini (makinikia).

Tangu ilipoanza uzalishaji nchini zaidi ya miaka 15 iliyopita, takwimu zinaonyesha kuwa kampuni hiyo imewekeza Dola 4 bilioni na kulipa kodi na mrabaha wa zaidi ya Dola 1 bilioni.