Rais Kenyatta, Odinga wabanana kura za maoni za Ipsos, Infotrack

Muktasari:

47%: Uhuru anaongoza kwa mujibu wa Ipsos.

47%: Odinga anaongoza kwa mujibu wa shirika la Infotrak.

Nairobi, Kenya. Matokeo yaliyotangazwa jana na Shirika la Utafiti la IPSOS yanaonyesha kuwa umaarufu wa mgombea urais kwa muungano wa upinzani (Nasa), Raila Odinga umepanda lakini ukifanyika uchaguzi leo Uhuru Kenyatta wa Jubilee atashinda kwa asilimia 47.

Utafiti huo unaonyesha umaarufu wa Odinga umeongezeka kutoka asilimia 42 Mei hadi kufikia asilimia 43 Julai yaani ongezeko la asilimia moja huku Kenyatta akibaki na asilimia 47.

Matokeo haya ni tofauti na yaliyotangazwa na Shirika la Infotrak lililoonyesha Odinga akipanda kutoka asilimia 43 Juni hadi 47 Julai wakati Kenyatta akishuka kutoka asilimia 48 Juni hadi 46.

Akitangaza matokeo hayo juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Infotrak, Angela Ambitho alisema huenda takwimu hizo zikabadilika, ikizingatiwa kwamba asilimia sita ya wapigakura hawajaamua upande ambao wataunga mkono na kuwezesha kupatikana mshindi raundi ya kwanza.

“Hii ni ishara kwamba tunaweza kumpata mshindi wa moja kwa moja katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo kwa kutegemea mikakati ambayo wagombeaji hao wawili wakuu watatumia kushawishi wapigakura hao,” alisema Ambitho.

Takwimu za utafiti zilizochapishwa na Ipsos zinaonyesha uchaguzi mkuu ukifanyika leo Odinga na mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, wangeongoza katika maeneo ya Pwani (asilimia 63), Nairobi (64), Nyanza (76) na Magharibi (56).

Rais Kenyatta na makamu wake William Ruto wangeongoza maeneo ya Kati (asilimia 88), Mashariki (49), Kaskazini Mashariki (62) na Rift Valley (65).

Pia utafiti huo umebaini Chama cha Jubilee ni maarufu zaidi kwa asilimia 44, huku Nasa kwa asilimia 42.

Jubilee imeongoza kwa umaarufu maeneo ya Kati (asilimia 84), Rift Valley (63), Kaskazini Mashariki (61) na Mashariki (44). Nasa inaongoza Nairobi (asilimia 57), Pwani (64), Magharibi (56) na Nyanza (76).