Familia ni taasisi ya kwanza katika kukabiliana ukosefu wa ajira nchini

Muktasari:

  • Ukosefu wa ajira ni janga linalowakabili vijana wengi duniani. Serikali za mataifa tofauti zimekuwa zikiweka mikakati kadhaa kukabiliana na changamoto hii. Lakini, inaelezwa kuwa familia ni taasisi ya kwanza kutengeneza mazingira rafiki kwa kijana ama kuajirika au kujiajiri. 

Ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ni changamoto kubwa katika nchi zinazoendelea hata zilizoendelea. Baadhi ya watu wanaamini ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka, saratani inayoitafuna nguvukazi au janga la ulimwengu.

Utafiti uliyofanywa na Chuo Kikuu cha Duke nchini Marekani mwaka 2013 kuhusu changamoto hiyo hasa kwa vijana katika nchi 30 duniani, unaonesha kuna zaidi ya vijana milioni 350 hawana ajira.

Tafsiri ya umri wa kijana unatofautiana kati ya taasisi moja na nyingine. Lakini Shirika la Umoja wa Mataifa na taasisi zake humtambua kijana kuwa ni mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35.

Ukosefu wa ajira kwa vijana umesababisha waishi maisha duni. Utafiti wa chuo kikuu hicho unasema asilimia 28 ya vijana waliokuwa na uwezo wa kufanya kazi mwaka 2013 walikuwa wanaishi chini ya Dola 1.25 ya Kimarekani ambayo ilikuwa wastani wa Sh1,600 kwa siku.

Ni kipato ambacho hakiwezi kumfanya kijana akidhi mahitaji yake ya kila siku hasa kwa kuzingatia gharama za maisha zinazoendelea kupanda kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali.

Katika utafiti huo, changamoto kadhaa zilibainishwa na wataalamu hao wakatoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana nazo kwa mustakabali wa jamii inayostahili ajira zenye staha.

Changamoto ya kwanza iliyobainishwa ni ukosefu wa ujuzi kati ya wahitimu wa ngazi tofauti na mahitaji ya waajiri. Utafiti ulionesha wastani wa asilimia 34 ya taasisi zilisumbuka kupata vijana wenye sifa na hazikuwa na mawasiliano na vyuo vya elimu ya juu kuhusu aina ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Vyuo vingi katika nchi 30 duniani zilizoshirikishwa kwenye utafiti huo vinatajwa kuzalisha vijana wenye ujuzi ambao kwa asilimia fulani sio mahitaji ya soko la ajira kwa wakati husika.

Suala jingine ni kutokuwa na uelewa wa namna ya kuchangamkia au kutafuta fursa za ajira pamoja na kukosekana kwa mbinu za ujasiriamali pindi vijana hao wanapotakiwa kuachana na ajira.

Utafiti huo ulitoa mapendekezo kwa ajili ya kutatua changamoto zilizobainishwa. Mosi, ulizishauri taasisi za ajira kuwekeza katika elimu kwa kuwasomesha vijana katika taasisi mbalimbali za elimu kisha kuwaajiri baada ya kuhitimu.

Vilevile, zilishauriwa kuwajengea vijana uwezo katika fani mbalimbali hasa kupitia vyuo vya ufundi na taasisi za elimu kuwapa ufahamu wa mbinu za ujasiriamali ili kuwawezesha kujiajiri.

Ukosefu wa ajira kwa vijana una madhara ya moja kwa moja katika kuendeleza uchumi wa mtu mmoja mmoja, taifa na dunia kwa jumla. Kijana mmoja katika nchi za mashariki ya kati alijichoma moto mwaka 2011 kwa sababu inayotajwa kuwa ni ukosefu wa ajira ambao ulifika asilimia 26.5 mwaka 2013.

Kasi ya ongezeko la watu katika nchi za Afrika haiendani na nafasi za ajira zinazotengenezwa kila mwaka. Mwaka 2013 nafasi za ajira zilizotengenezwa zilikuwa milioni 74 sawa na asilimia 33 ya mahitaji.

Ukosefu wa ajira hasa kwa vijana unapaswa kuwa na mjadala wa kitaifa utakaowahusisha vijana kwa kiasi kikubwa. Vijana wanapaswa kushiriki na kushirikishwa katika malengo, dira na maono ya nchi yao.

Pamoja na mambo mengine taasisi za elimu ya juu na vyuo vya ufundi vinapaswa kuwa na mfumo wa kufuatilia vijana wanaohitimu katika taasisi zao ili kubaini endapo masomo wanayofundisha yanakidhi mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri.

Serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto ya ajira kwa vijana hivyo kuhitaji ushiriki wa taasisi binafsi na mash yanapaswa kushirikiana katika kupunguza changamoto hiyo.

Licha ya taasisi hizo za kijamii na umma, familia ni nguzo muhimu ya kujenga ujasiriamali kwa watoto. Kuanzia akiwa mdogo, mtoto anapaswa kujengewa uwezo wa kujitegemea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Hili linapaswa kufanywa kwa kumpa maarifa ya kutafuta fedha zake, kutumia kwa busara, kutunza na kuwekeza kwenye mradi utakaompa faida ya kutosha kukidhi mahitaji yake.

Wananchi wengi nchini hawana elimu ya fedha jambo linaloongeza changamoto ya kupangilia mambo yao kwa ufasaha na kujikomboa kiuchumi. Kabla ya watu wengine, familia inapaswa kujenga msingi imara kwa watoto.

Zipo akaunti za watoto ambazo zinaweza kufunguliwa muda wowote baada ya mtoto kuzaliwa, ni sehemu nzuri ya kuanza kumfundisha kujihusisha na taasisi za fedha ili azitumie kwa biashara zake hapo baadaye.

Mzazi au mlezi anayeenda benki na mwanaye mdogo kuweka au kutoa fedha kisha akamuelewesha kuhusu kilichofanyik ani tofauti na mtoto ambaye atakuja kuzijua huduma za benki baada ya kujiunga chuo kikuu kama ilivyo kwa wengi.

Mkakati huu ukianzi ahuko, hakika itasaidia kupunguza idadi ya vijana wanaolalamika kukosa ajira kwani wapo watakaojiajiri.