Serikali yatangaza bei mpya ya unga Dar

Muktasari:

“Kila aliyepewa mahindi amepewa mkataba wenye maelekezo kwamba auze unga kwa bei ya Sh900 kwa kilo na tutafuatilia ili kuona bei ya unga inashuka,”

BEI ya unga wa sembe mkoani Dar es Salaam inatarajia kupungua kutoka Sh1,500 hadi 900 kwa kilo kuanzia wiki hii baada ya tani 3056 za mahindi kuanza kukobolewa.

Serikali ilitoa vibali kwa wenye vinu vya usagishaji kuchukua mahindi kwenye maghala ya kitaifa  kwa ajili ya kupunguza makali ya bei za vyakula kupanda.

Mkoa wa Dar es Salaam ulipata mgao wa tani 6,400 kutoka wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na hadi sasa tani 3056 za mahindi zimetolewa kwa wafanyabiashara hao walioingia mkataba na Serikali kuuza unga bei ya rejareja Sh900.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Denis Nyakisinda alisema tani hizo zimegawanywa katika wilaya tatu za mkoa huo ambapo Kinondoni imepata tani 3,600 wakati Temeke na Ilala zimepata tani 1,400 kila moja.

Alisema Wilaya ya Kinondoni imepewa tani nyingi kwa sababu kuna mashine nyingi na kwamba Tandale na Manzese ndiyo inayolisha Dar es Salaam.

“Kila aliyepewa mahindi amepewa mkataba wenye maelekezo kwamba auze unga kwa bei ya Sh900 kwa kilo na tutafuatilia ili kuona bei ya unga inashuka,” alisema Nyakisinda na kuongeza kuwa:

“Kuna baadhi ya maeneo kama ya Mbagala ambako kuna wafanyabiashara walishachukua mahindi hivyo tunategemea bei ya unga itapungua baada ya mahindi kuingia sokoni na kukobolewa,” alisema.

Alisema hadi sasa kuna wafanyabiashara 48 ambao wamepewa vibali kwa ajili ya kwenda kununua mahindi hayo katika maeneo ya Songea, Makambako na Mbozi na kwamba wafanyabishara hao ni wale wa kati, wadogo na baadhi ya makampuni makubwa.

Alisema mchakato wa kuwapata wafanyabiashara hao ulifanyika kwenye wilaya kwa kupitia kwa watendaji wa mitaa ambako mashine zipo na kwamba baada ya hapo mkoa ulipokea majina na kuyatuma Wakala wa Chakula (NFRA) kwa ajili ya kupewa vibali.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, Songea zimetengwa tani 4200 ambapo wafanyabiashara watakaokwenda kuchukua huko watauziwa kwa bei ya Sh460 kwa kilo wakati Mbozi zimetengwa tani 1800 na wafanyabiashara watauziwa Sh490 kwa kilo na Makambako ziko tani 400 ambazo wafanyabiashara watauziwa Sh500 kwa kilo.

Alisema mfanyabiashara atakayekiuka mkataba atachukuliwa hatua za kisheria kwani wamejipanga kufuatilia kwa kila mfanyabiashara aliyepewa kibali na kwamba kila wanaposhusha mzigo lazima wapige simu kwa maofisa kilimo wa maeneo husika.