Friday, October 23, 2015

Kampuni zateketeza dawa za Sh92 milioni

 

By Hawa Mathias, Mwananchi

Mbeya. Kampuni tatu za maduka ya dawa za binadamu mkoani Mbeya zimeteketeza dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya Sh92 milioni baada ya kuzipeleka kwenye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Mkoa wa Mbeya, Dk Silvester Mwidunda alisema jana kuwa kampuni hizo ziliwajibika zenyewe kukusanya dawa hizo na kuziwasilisha kwao ili ziteketezwe.

Dk Mwidunda alisema kwa mujibu wa Sheria ya Dawa ya Mwaka 2003 kila mfanyabiashara wa maduka ya dawa na vipodozi anapaswa kusalimisha bidhaa zilizokwisha muda.

Alisema mbali na dawa, TFDA pia iliteketeza vipodozi vyenye thamani ya zaidi ya Sh8 milioni vilivyokamatwa katika maduka mbalimbali jijini hapa.

Mkaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini , Yusto Wallace alisema kuna changamoto kubwa ya uingizwaji holela wa dawa na vipodozi hali inayochangiwa na ushirikiano hafifu katika mipaka ya Malawi na Zambia.

Alisema kutokana na changamoto hiyo wameweka mikakati ya kufanya mikutano ya ujirani ili kuona namna kutokomeza bidhaa hizo.

Mfanyabishara wa duka la madawa muhimu, Ditram Kutemile alisema ili Serikali iweze kufikia malengo ni lazima itoe elimu kwa wafanyabishara katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani.

Alisema hiyo itasaidia kupunguza utitiri wa dawa na vipodozi bandia au vilivyokwisha muda wake kuingizwa kwenye soko.

Friday, October 23, 2015

Intaneti zafungwa Congo Brazzaville

 

Brazzaville, Kongo. Serikali ya Congo Brazzaville imesitisha huduma za mtandao na kufunga mawimbi ya redio ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI) nchini humo.

Pia, Serikali imetangaza kusimamisha huduma nyingine za mawasiliano ikiwamo ujumbe mfupi wa simu katika hatua zake za kukabiliana na wimbi la maandamano yanayoratibiwa na wapinzani.

Hatua hizo zimechukuliwa ikiwamo imepita siku moja, baada ya watu wanne kuuawa mjini Brazzaville katika makabiliano baina ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani wanaopinga kura ya maoni kuhusu katiba mpya.

Wapinzani wamekuwa wakiandamana kupinga vikali kura ya maoni ya katiba mpya ambayo inampa Rais Dennis Sassou Nguesso uwezo wa kugombea urais nchini humo katika uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika baadaye mwaka 2016.

Kwa mujibu wa katiba ya sasa, Rais Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 72 hawezi kugombea urais kwa mara nyingine.

Katiba inaeleza kwamba hawezi kugombea urais kwa sababu amemaliza mihula yake miwili.

Hata hivyo, katika katiba mpya iliyopendekezwa vizingiti hivyo viwili vimeondolewa na hivyo kumfungulia njia kiongozi huyo wa siku nyingi kugombea tena nafasi ya urais ili kurudi madarakani.

Rais Nguesso alikuwa rais tangu mwaka 1979 hadi 1992.

Baadaye alikuwa kiongozi wa upinzani na kurejea madarakani baada ya vita vya ndani nchini humo mwaka 1997 vilivyogharimu maisha ya raia wadhaa.

Wiki iliyopita Serikali ilitangaza kuyapiga marufuku maandamano yaliyoitishwa na wapinzani waliokuwa wakimpinga Rais Nguesso kutaka kuendelea kukaa madarakani kwa awamu ya tatu.

Wapinzani hao wanataka kuheshimiwa kwa katiba iliyopo na wametishia kuendelea na maandamano iwapo jaribio hilo la kurekebisha katiba halitasitishwa na serikali iliyopo madarakani.

Hivi karibuni wakati akiwa nchini Ethiopia, Rais Barack Obama wa Marekani aliwaonya baadhi ya viongozi wa Afrika wanaopenda kubadili katiba ili waendelea kusalia madarakani.

Alisema kuwa hali kama hiyo siyo tu inakwamisha ukuaji wa demokrasia lakini pia inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kwa hivi sasa kumekuwa na vuguvugu linaloendelea katika baadhi ya nchi kutaka kubalisha katiba ili viongozi walioko madarakani waendelee kusalia madarakani.

Tayari nchini Rwanda bunge limepitisha muswaada unaotaka kuitishwa kwa kura ya maoni ili kumwezesha Rais Paul Kagame kuwania muhula mwingine.

Pia, kumekuwa na vuguvu lingine katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutaka kurekebisha sehemu ya vipengele vya katiba ili kutoa nafasi kwa Rais Joseph Kabila kuwania muhula mwingine wa uongozi. Wapinzani wamekuwa wakikosoa vikali hali hiyo.

Friday, October 23, 2015

Kumbi za starehe, michezo zafungwa kunusuru uchumi ZambiaRais wa Zambia, Edgar Lungu

Rais wa Zambia, Edgar Lungu 

Lusaka , Zambia. Rais wa Zambia, Edgar Lungu amemwomba Mungu kuinusuru nchi yake dhidi ya kuendelea kuporomoka kwa thamani ya fedha nchini humo, huku mamlaka husika zikichukua hatua zaidi kukabiliana na halihiyo.

Serikali ya nchi hiyo imetangaza kufungwa kwa kumbi zote za burudani huku mechi zote za mpira zikiahirishwa kupisha siku maalumu ya kuliombea taifa.

Kiongozi huyo alitangaza hatua hiyo wiki iliyopita baada ya thamani ya fedha kuanguka kwa asilimia 45 dhidi ya Dola ya Marekani. Hali hiyo ilisemekana kuchangiwa na kuanguka kwa bei ya madini ya shaba ambayo ni tegemeo lake kuu la kiuchumi.

Bei za vyakula pia zimepanda pia uzalishaji wa umeme umepungua kutokana na kiwango kidogo cha maji katika Ziwa Kariba. Ziwa hilo linategemewa kwa uzalishaji wa umeme.

Kwa mujibu wa Shirika la Utafiti la Bloomberg Service, thamani ya Kwacha imeshuka zaidi dhidi ya Dola ya Marekani katika nchi zote 155 ilizozifanyia utafiti.

“Mungu wetu amesikia vilio vyetu. Ametusamehe dhambi zetu na tuna imani kuwa ataiponya nchi yetu kutokana na changamoto hii kubwa ya kiuchumi,” alisema Rais Lungu wakati alipokuwa akilihutubia watu zaidi ya 5,000. Marais wa zamani, Kenneth Kaunda na Rupiah Banda pia walihudhuria hafla hiyo.

“Hatupaswi kutafuta upenyo wa kisiasa kutokana na changamoto zetu .zinazotukabili kwani wanaoumia ni watu wetu” alisema Rais Lungu.

Friday, August 5, 2011

Museveni aitisha kikao cha dharura kujadili Uchumi

KAMPALA,Uganda,BBC
RAIS Yoweri Museveni amelazimika kuitisha  kikao cha dharura cha mawaziri kujadili jinsi ya kukabili hali mbaya ya uchumi nchini humo.

Baraza hilo la mawaziri linakutana katika kipindi ambacho viongozi wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za maisha.

Bidhaa muhimu kama vile sukari zimeanza kukosekana madukani hali ambayo inawaathiri watu wenye kipato cha chini nchini humo.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala alisema bei ya sukari imepanda kiasi kwamba kile kiasi kilichoko aidha kinafichwa ama kuniauzwa bei kali ambayo sio ile ya kawaida.

katika maduka makubwa watu hawakubaliwi kununua zaidi ya kilo moja.

Hali hii inatishia uchumi wa taifa ambao kwa sasa kwa mujibu wa gavana wa benki kuu ya taifa kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Uganda kitadidimia kwa asilimia 5 kutokana na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei za bidhaa.
Mfumuko wa bei unakaribia asilimia 20, kiwango kikubwa zaidi kwa kipindi cha miaka 10.

Pia kiwango cha ubadilishanaji wa pesa za Uganda kwa dola kumepanda kiasi kuwa dola 1 inanunua shilling za Uganda 2,634.

Msemaji wa serikali na waziri wa habari Mary Okurut alisema kikao hicho maalum cha mawaziri kitajadili mikakati ya kukabili hali hii ya uchumi.

Kuhusu kutoweka kwa sukari madukani, waziri Okurut amesema kuwa serikali imeomba ruhusa kutoka jumuiya ya Afrika mashariki ikubaliwe kuagizia sukari kutoka nje ya ukanda huu.

Uganda ina viwanda vitatu vinavyozalisha sukari, lakini ni kimoja tu kwa sasa kinachofanya kazi.
Viwili vilivyosalia, kimoja kimefungwa kwa sababu mitambo yake inafanyiwa ukarabati ilhali kingine kwa kuwa hakipati miwa inayotosheleza uzalishaji

Wakati huo huo Shirika  la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetahadharisha kuwa Uganda pia inaelekea kukumbwa na baa la njaa ambalo linashuhudiwa hivi sasa katika nchi za Pembe ya Afrika.

Msemaji wa shirika la FAO alisema kuwa, kutokana na kuelekea kumalizika akiba ya chakula nchini Uganda, usalama wa chakula kwa taifa hilo upo hatarini na huenda wananchi wake wakapatwa na yale yanayoshuhudiwa hivi sasa katika nchi za Somalia, Kenya, Ethiopia na Djibouti.

Friday, August 5, 2011

UN yatajwa uhalifu wa mtandao

WASHINGTON, Marekani AFP
UMOJA wa Mataifa( UN), Mashirika Makubwa  na Serikali mbalimbali duniani   zimetajwa kuhusika katika matukio ya uhalifu kwa kutumia mtandao wa Internet.

Hiyo ni kutoka na utafiti uliofanywa na kampuni inayojihusisha na masuala ya usalama wa Kompyuta McAfee ambao wamekuwa wakichunguza vitendo hivyo.

Kampuni hiyo iligundua zaidi ya wahanga 72, ambao  tayari walishaathirika na uhalifu huo kupitia njia hiyo ya mtandao wa internet.

Kampuni hiyo ilitaja Mashirika makubwa ukiwemo Umoja wa Mataifa  kwa kuwa wakuu wa moja kati ya matukio makubwa kabisa ya uhalifu kupitia  katika mtandao wa internet.

Pia ilizitaja Serikali za Marekani,Canada, India na Korea Kusini pamoja na mashirika makubwa kama vile kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kwamba  ni miongoni pia mwa wale waliyokabiliwa na matukio hayo.

Kampuni hiyo ya McAfee hata hivyo haikutaja wale ambao inadhani wanahusika na vitendo hivyo vya uhalifu wa mtandao, lakini kuna wasi wasi kuwa huenda China ikawa inahusika.

Awali wizi wa mtandao ulitawala sana hususan katika mabenki duniani huku ukisababisha hasara za mabilioni ya pesa.

Inasemekana pia wanaotumia wizi wa aina hiyo ni wale wezi wa kimatifa ambao pia wanauwezo mzuri wa kucheza na masuala ya komputa vilivyo.
 
Wakati huo huo 
Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa limetangaza mikoa mitatu zaidi nchini Somalia kuwa inakabiliwa na baa kubwa la njaa.

Shirika hilo katika taarifa yake lilisema kuwa kwa hali inavyoonekana baa hilo litaendelea hadi mwisho wa mwaka huu.

Aidha Umoja wa Mataifa ulisema idadi ya vifo vya wakimbizi wa kisomalia wanakimbilia Kenya, inazidi kuongezeka.
Baa hilo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa linaonekana kuwa kubwa kulizidi lile lililoikumba Somalia mwaka 1992.

Mikoa hiyo mipya mitatu iliyotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa katika hali mbaya huko Somalia ni pamoja na  Afgoye, Shabelle ya kati na mji mkuu Mogadishu, ambako wiki iliyopita waasi wa Al Shabaab walipambana na kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM kinachoiunga mkono serikali ya mpito nchini humo.

Mkoa wa Afgoye pekee una zaidi ya wasomali laki nne, na hivyo kuufanya kuwa na kambi kubwa kabisa duniani ya watu wasiyo na makaazi pamoja na kuwepo kwa juhudi kubwa zinazofanywa na makundi ya kutoa misaada.
Mjini Washington, Seneta Chris Coons alisema kuwa  mamia kwa maelfu ya watoto wanakabiliwa na kifo katika eneo lote la pembe ya Afrika, ikiwemo Ethiopia.

Alisema ni nusu tu ya dola billioni mbili zinazohitajika na Umoja wa Mataifa kusaidia hali hiyo ndizo zilizoahidiwa na mataifa wahisani

Monday, July 11, 2011

Mataifa yaahidi kuimwagia misaada lukuki Sudan Kusini

JUBA, Sudan Kusini
MATAIFA mbalimbali duniani yameahidi kuisadia nchi mpya ya Sudan Kusini baada ya kujitenga na kuwa taifa huru.
Misaada pia itawezesha taifa hilo jipya kuanzisha mfumo imara wa kisiasa pamoja na kuwa na maendeleo lukuki nchini humo.

Rais wa China, Hu Jintao jana ametoa pongezi lukuki mjini Beijing kwa nchi ya Sudan Kusini kuwa huru na ameahidi kushirikiana na nchi hiyo pamoja na kuingia mkataba nayo katika masuala ya usambazaji wa mafuta.

China ambayo ni mnunuaji wa mafuta ya Sudan na alikuwa anahakikisha kuwa kutengana kwa sehemu hizo mbili hakutaleta madhara katika ununuaji wa mafuta katika nchi yake.

Katika hotuba yake ya kila wiki kupitia kanda ya video, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel jana alisema kuwa baada ya Sudan Kusini kujitenga na kuwa taifa jipya, nchi yake itaisaidia nchi hiyo ili iwe na mfumo bora wa kisiasa.

“Sasa ni muhimu kuiunga mkono Sudan Kusini, kuelekea utulivu utakaowaletea watu wa eneo hilo amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi,” alisema Merkel.

Hata hivyo, kuanzia leo Jumatatu, Kansela Merkel anatarajia kulitembelea bara la Afrika kwa mara ya pili aikiwa ni kiongozi wa serikali, kuanzia leo hadi siku ya Alhamisi.
Kiongozi huyo anatarajia kuzitembelea Kenya, Angola na Nigeria.

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alisema umoja huo umeunda kikosi kipya kwa ajili ya Sudan Kusini cha kusaidia kuimarisha amani pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya kimaendeleo nchini humo.
Pia alizisihi nchi za Sudan na Sudan Kusini kushirikiana.

Alisema nchi hizo ni kama ndugu hivyo licha ya kutengana, ushirikiano ni muhimu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
 “Ni nafasi ya kuthibitisha tena ahadi ya kujenga uhusiano wa amani, wenye manufaa na kukabili hatima yao kama washirika - siyo washindani," alisema Ban Ki-moon.

Aliongeza kwamba, pande hizo mbili hazijafikia muafaka juu ya namna ya kugawana mafuta na mapigano yamezuka katika maeneo ya mpaka baina yao.

Nayo Marekani, kupitia balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice alisema Marekani ipo bega kwa bega taifa hilo jipya na itahakikisha inashirikiana vizuri na nchi hiyo.

Kabla ya sherehe za uhuru huo, Ikulu ya Marekani ilimteua Rice kuongoza ujumbe wa nchi hiyo katika sherehe hizo za uhuru.

Katika sherehe hizo ambazo ziliungwa mkono na Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ambapo aliuambia umati ulioudhuria sherehe za uhuru na viongozi wa kimataifa, kwamba Sudan imetimiza ahadi yake.

Alisema wengi hawakuamini kuwa Khartoum itaiacha Sudan Kusini yenye utajiri wa mafuta, ijitenge.

"Ni wakati wa Marekani nayo kutimiza ahadi yake, na iondoshe vikwazo dhidi ya Sudan,” alisema Rais Bashir.
Vikwazo hivo vinaleta shida kwa uchumi wa Sudan, ambayo sasa, baada ya Sudan Kusini kupata uhuru, pia imepoteza mafuta mengi.

Rais Bashir piya alitoa wito kuwepo uhusiano wa amani na Sudan Kusini, lakini alikiri kuwa usalama kwenye mpaka wa karibu kilomita elfu mbili baina yao, utakuwa changamoto kubwa.

Uhuru wa Sudan Kusini umetokana na mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mingi.

Sudan Kusini inakuwa taifa la 193 duniani, na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, na pia kuwa taifa la 54 barani Afrika.

Naye Salva Kiir Mayardit ambaye amekubaliwa na wananchi wa taifa hilo kuingoza nchi hiyo alitoa kipaumbele cha kuboresha miundombinu nchini humo ikiwa ni pamoja na ushirikiano.
REUTERS

Wednesday, April 20, 2011

Benki ya Dunia kuboresha elimu nchi zinazoendelea

Hadija Jumanne
BENKI ya Dunia (WB) inatarajia kuboresha elimu kwa nchi zenye kipato cha chini ili kutoa elimu bora kwa wote huku ikiwekeza katika ujuzi na maarifa yatakayopatikana.

Pia itafanya kazi kwa pamoja na nchi hizo ili kuziendeleza sera ambazo zitarahisisha upatikanaji wa elimu duniani.

Aidha, benki hiyo imetoa msaada wa dola 750 milioni za Kimarekani kwa nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika na zilizo kusini mwa Asia ili kusaidia nchi ambazo mpaka kufikia mwaka 2015 zitakuwa hazijafikia kiwango cha elimu ya maendeleo ya milenia   .

Taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa na Wizara ya Fedha ikimnukuu msemaji mkuu wa Benki hiyo, ilisema katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Benki ya Dunia iliwekeza dola 69 bilioni za Marekani katika sekta ya elimu  ambayo ni zaidi ya miradi 1500.

Mwaka 2010 benki  hiyo iliingia mkataba mpya wa zaidi ya dola 5 bilioni za Marekani ili kusaidia kuimarishwa kwa sekta ya fedha.

Taarifa hiyo ilisema kuwa sekta binafsi ziliwekeza katika ushirikiano wa fedha wa kimataifa hadi kufikia dola 170 milioni za Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ili kuzisaidia nchi kufikia kiwango cha elimu ya maendeleo ya milenia, Benki Kuu itaongeza  misaada katika elimu ya awali kiasi cha dola 750 milioni za Marekani ambapo pesa hizo zitasaidia nchi ambazo mpaka kufikia mwaka 2015 zitakuwa hazijafikia kiwango cha elimu ya maendeleo ya milenia hasa  kwa nchi kusini mwa  Jangwa la Sahara, barani Afrika na zilizo Kusini mwa Asia.

Alisema misaada mingine itakayo tolewa na Benki ya Dunia ni pamoja na kuboresha na kurahisisha upatikanaji wa elimu bora kwa watu waliopo ili kukidhi mahitaji kwa wote wanaohitaji huduma hiyo.

Tuesday, April 19, 2011

Afrika Mashariki kutoa ajira 23,000

Salma Said, Zanzibar
IMEELEZWA kwamba nchi za Tanzania , Kenya na Uganda zinatarajiwa kupata ajira mpya 23,000 baada ya miaka mitano ijayo.Ajira hizo zitatarajiwa kuwanufaisha  1.2 milioni  ili kukabiliana na hali ya maisha na kuondokana na umaskini.

Hayo yalielezwa na mtaalamu wa mpango wa kukuza ujasiriamali, Julius Mutio, kutoka nchini Kenya wakati akizungumza katika semina ya siku moja iliyotayarishwa na taasisi uanzishaji na ukuzaji wa shughuli za ujasiriamali kwa vijana (YEF) Shangani Zanzibar.

Mutio alisema ajira hizo zinatarajiwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo baada ya utekelezaji vipengele sita vya kufikia malengo ya mpango huo kukamilika.

Alisema vipengele vinavyotekelezwa kwa sasa ili kuwezesha kufikiwa kwa lengo hilo, ni pamoja na kazi ya kutambua asasi za kiraia zinazohusika na maendeleo ya vijana na kuzishirikisha katika mpango huo kwa kuziwezesha kutoa elimu ya kuamsha upeo wa vijana kuingia katika ujasiriamali wa ushindani.

Mpango huo utakapokamilika na kupatikana ajira hizo itakuwa ni sehemu ya malengo ya Tume ya Maendeleo ya Afrika, unaolenga katika kukuza ajira kwa vijana na kupambana na umaskini kupitia sekta ya ujasiriamali katika nchi hizo.

Naye Ofisa wa Elimu ya Ushirikishi na Mawasiliano wa YEF, Miriam Christensen alisema mpango huo utatekelezwa kwa miaka mitano kwa ufadhili wa awali wa dola 24 milioni za Marekani kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Denmark (DANIDA) na Tume ya Maendeleo ya Afrika.

Akizungumza kwa upande wake katika semina hiyo ,Mratibu wa mpango huo kwa upande wa Tanzania, Mkuku Louis alisema asasi za kiraia 27 kati yake 20 Tanzania bara na saba Zanzibar ambazo zinahusika na maendeleo ya vijana Tanzania bara na Zanzibar ,  zimechaguliwa hapa nchini baada ya kukidhi sifa za kushiriki katika utekelezaji wa mpango huo.

Louis alisema hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo kwa upande wa Tanzania imekamilika kwa kutambua asasi za kuingia katika mpango na kazi inayofuata ni kutoa elimu kwa asasi hizo juu ya namna ya kuamsha upeo wa vijana kuingia katika ujasiriamali wa usindikani na uzalishaji mali.

Monday, April 4, 2011

Jubilee yapata faida ya KSh.2 bilioni

Nairobi,
KAMPUNI kongwe kabisa ya bima katika nchi za Afrika Mashariki ya Jubilee Holdings, imepata faida ya Sh2.053 bilioni za Kenya katika kipindi cha mwaka jana kutoka Sh1.116 bilioni mwaka za mwaka juzi.

Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 84 kabla ya kodi katika mwaka ulioishia Desemba 31, mwaka jana.
Kutokana na faida hiyo, kampuni imetoa gawiwo la asilimia 110 kwa wanahisa ambalo ni sawa na Sh5.50 za Kenya kwa kila hisa.

Kwa upande wao, wakurugenzi pia wametoa toleo la hisa za bonasi kwa wanahisa kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya  kampuni kutengeneza faida.Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Jubilee Holdings, ilisema  toleo la hisa za bonasi limetolewa kuadhimisha miaka 75 tangu  kuanzishwa kwa kwa kampuni hiyo.

Kampuni ya Jublee Holdings, ilianzishwa mwaka 1937 ikiwa kampuni ya kwanza ya bima, katika nchi za  Afrika Mashariki. Katika mwaka 2010 imefanya biashara iliyofikia Sh10 bilioni za Kenya ambayo ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na pato la mwaka 2009.

Bima ya maisha ilikua kwa kiwango kikubwa zaidi cha asilimia 42 wakati bima za muda mfupi zilizongeka kwa asilimia 24 ambazo kwa pamoja zilichangia ukuaji wa biashara wa asilimia 33 pamoja na ongezeko la asilimia 28 katika bima ya afya.

Kampuni ya Jublee  ilisema katika taarifa yake kuwa mwaka 2010 bima za kinga ziliongezeka kwa asilimia 42 na kuingiza faida ya Sh523 milioni za Kenya kutoka Sh367 mwaka 2009.
Ilisema katika kipindi cha mwaka jana, mali za kampuni zilikua na kufikia thamani ya Sh31.652 milioni za Kenya kutoka mali za thamani ya Sh24.874 za Kenya  mwaka 2009.

Kuhusu biashara za muda, taarifa hiyo inasema ilikuwa kwa wastani wa asilimia 28 wakati bima za maisha zilikuwa kwa asilimia 42 mwaka 2010. Ongezeko hilo lilichangiwa na mkakati wa kampuni wa kutoa elimu ya umma kwa lengo la kukamata soko katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Kampuni imepata mafanikio na kushika kiwango kikubwa cha soko katika biashara kwa jumla kwa asilimia 33, wakati katika bima ya afya kwa asilimia 23 na katika bima ya maisha inashika asilimia 43 soko na hivyo kuongoza katika soko la  Kenya.
Mwenyekiti wa Jubilee Holdings, Nizar Juma, amesifu mafanikio yaliyopatikana.
"Tunafurahia sana kwani kampuni imezidi kupata mafanikio na kuongoza katika soko la Kenya," alisema.

Monday, December 6, 2010

Iran yaanza mzungumzo kuhusu mpango wa Nyuklia

GENEVA, Uswisi
IRAN imeanza mazungumzo na nchi za Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani kuhusu mpango wake wa nyuklia, mazungumzo ambayo yanadhaniwa kuwa hayatakuwa na matokeo ya kuridhisha.
Mkutano huo unaotarajiwa kumalizika leo, utaashiria kumalizika kwa kwa miezi 14 ya kusita kwa mazungumzo hayo, kwa sababu ya hatua ya Iran kukataa pendekezo la kuacha kurutubisha madini yake ya uranium ili ipewe nishati ya nyuklia.

Mpatanishi mkuu wa Iran katika mzozo huo, Saed Jalili aliwasili juzi mjini Geneva, akiwa ameandamana na naibu wake Ali Begheri na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Ahani.
Ingawa mataifa sita yanakutana na Iran kwenye meza ya mazungumzo, ajenda ya mazungumzo hayo bado haijawekwa wazi,  siku chache zilizopita Iran ilitaka ajenda ya mazungumzo ielezwe kwanza kabla kuhudhuria mikutano katika siku za usoni.

Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, mwishoni wa juma lililopita, rais wa Iran Mahmoud Ahamedinejad alisisitiza tena kwamba Iran haitakubali kuachana na mpango wake wa nyuklia na kusema mipango ya kurutubisha uranium sio suala la kujadiliwa.

"Tunatumia tu haki yetu kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia. Hatuzidishi wala hatupunguzi hata kidogo." Alisema Nejad.
Kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, Iran ina haki ya kutumia madini ya uranium kwa matumizi ya amani na kutumia ujuzi wa Atomiki.
Pia mkutano huo umekuja siku moja tu baada ya Iran kusema kuwa imepiga hatua kubwa mbele katika mpango wake wa nyuklia, hivyo kuashiria kuwa haina nia ya kuachana na mpango wake huo, ambao inasisitiza ni kwa ajili ya matumizi ya amani ya uzalishaji wa nishati.
DW

-->