CRDB yageukia Vicoba, harusi

Muktasari:

  • Utaratibu huo waelezwa kuwa utasaidia kuondoa mwanakikundi au mweka hazina kuondoka na fedha

Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka kwa matukio ya wizi wa fedha unaochangiwa na kukosekana kwa uaminifu kwa wanavikundi vya kujikwamua kiuchumi, Benki ya CRDB imebuni bidhaa tatu mpya ikiwamo akaunti ya Vicoba kupata akaunti kupitia simu ya mkononi ili kuondokana na changamoto zinazowakabili.

Suluhisho hilo limebainishwa na meneja wa huduma za mtandao wa CRDB, Edith Metta alipotoa elimu kwa wanahabari kuhusiana na huduma hizo mpya kwa wateja.

Kwa siku za karibuni, Metta alisema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya vikundi kupoteza fedha kutokana na wizi au mmoja kukimbia nazo hali hiyo ilisababisha benki hiyo kuja na suluhisho.

Alizitaji huduma hizo mpya kuwa ni akaunti ya kikundi, akaunti ya akiba na akaunti ya malipo.

Kwa wanachama wa Vicoba alisema wanaweza kufungua akaunti ya pamoja kupitia simu za mkononi kisha kusajili jina la kikundi na kuanza kuweka na kutoa fedha bila makato yoyote.

“Mwanachama ana uwezo wa kuangalia salio lililopo katika akaunti ya kikundi na iwapo kuna fedha imetolewa kinyemela akajua,” alisema.

Metta alisema akaunti hiyo inahakikisha fedha zinakuwa salama na iwapo kuna udanganyifu umefanywa na yeyote wanakikundi wanajua mapema.

Akaunti hiyo inatoa mwanya kwa wanachama kuanzia watatu hadi 3,000 wanaoweza kutunza mpaka Sh50 milioni, huku kukiwa na fursa ya kupata mikopo kwa kikundi kitakachokuwa na kumbukumbu nzuri za utunzaji fedha.

Licha ya Vicoba, alisema akaunti hiyo inazifaa kamati za harusi pia kwa kuwahamasisha wachangiaji wote kufanya malipo kupitia akaunti ya kikundi na fedha zao zikawa salama kuliko kumuachia mweka hazina kwenda nazo nyumbani kwake.

“Kuliko mtu aende benki kutoa fedha ya mchango au mweka hazina kupata shida ya kuweka kumbukumbu za wachangiaji, ukihamisha fedha kwenda akaunti hii salio litaongezeka hivyo kuondoa haja ya kuandaa taarifa ya fedha,” alisema Metta.

Kupata taarifa za akaunti kupitia simu ya mkononi, alisema mteja atatakiwa kubonyeza *150*62# na kufuata maelezo akitumia kitambulisho cha mpigakura au cha taifa. Mchakato huo unakamilika ndani ya dakika mbili.

Metta alisema lengo la huduma hiyo ni kuwafikia wateja wengi hususan waliopo maeneo ya vijijini ambao wamekuwa wakihifadhi fedha zao katika mfumo usio rasmi jambo linalohatarisha usalama wa fedha hata wao wenyewe.

Alisema huo ni miongoni mwa ubunifu wa kukomesha uhalifu.