Dk Tizeba awaonya wakaguzi wa viuatilifu, awataka kujitathmini

Muktasari:

  • Dk Tizeba alisema kitendo cha wakaguzi kuomba rushwa bila woga kinasababisha wananchi kuumia kutokana na kutumia viuatilifu visivyo sahihi.

Morogoro. Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amekemea tabia ya baadhi ya wakaguzi wa viuatilifu hasa waliopo mipakani kuomba rushwa.

Dk Tizeba alisema kitendo cha wakaguzi kuomba rushwa bila woga kinasababisha wananchi kuumia kutokana na kutumia viuatilifu visivyo sahihi.

Alisema hayo juzi mjini Morogoro alipofungua mafunzo ya wakaguzi wa viuatilifu kutoka maeneo ya mipakani ya Mtwara na Tunduma pamoja na Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Mtwara; na Bandari ndogo ya Kigoma. Pia, mafunzo hayo yaliwashirikisha wataalamu wa kanda tano za kilimo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI).

Alisema umefika wakati kwa wizara kupitia vitengo vyake kuangalia namna ya kupata watumishi wenye uelewa wa kina juu ya viuatilifu kwa kuwa, wengi waliopo vituo vya ukaguzi hasa mipakani hawana weledi.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa TPRI, Dk Margaret Mollel alisema jukumu la taasisi yake ni kusajili viuatilifu vyenye viwango vilivyokusudiwa kihalali na kusimamia matumizi sahihi kwa kutoa mafunzo kwa wakulima, maofisa ugani na wataalamu wengine wa Wizara ya Kilimo.

Dk Mollel alisema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wakaguzi kutokana na kupungua baada ya kustaafu na wengine kuacha kazi.

Kaimu msajili wa viuatilifu ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo, Habibu Mkaranga alisema kwa mujibu wa Sheria namba 13 ya mwaka 1997 ya Hifadhi ya Mimea, wakaguzi wanatakiwa kufanya ukaguzi wa viuatilifu, lakini ni lazima wasajiliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Mkaranga alisema kutokana na baadhi ya wakaguzi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya viuatilifu, TPRI imeanza kutoa mafunzo kwa wakaguzi waliopo ili waweze kujua sheria na utaratibu wa ukaguzi.