Gondwe: Ole wao wauza mbegu bandia

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe

Muktasari:

Kauli ya Gendwe ilitokana na malalamiko ya wakulima kwamba walinunua mbegu za ruzuku ambazo hazikuota na kusababisha kupata hasara na isitoshe kwa sasa wanakabiliwa na njaa.

Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ameahidi kupambana na matapeli wa mbegu za mahindi ambao wamewasababishia hasara wakulima wilayani humo.

Kauli ya Gendwe ilitokana na malalamiko ya wakulima kwamba walinunua mbegu za ruzuku ambazo hazikuota na kusababisha kupata hasara na isitoshe kwa sasa wanakabiliwa na njaa.

“Kuanzia leo, kampuni itakayohusika na usambazaji wa mbegu bandia, tutaichukulia hatua kali ili. Ni lazima wajue Serikali hii ya Mheshimiwa (John)Magufuli haina masihara na watu wanaowadhulumu watu wa kipato cha chini,“ alionya Gondwe kwenye mkutano na wakulima wa Kabuku.

Hata hivvyo, aliwataka wakulima kuhakikisha wanapewa risiti wakati wanauziwa mbegu hizo ili iwe rahisi kwa Serikali kufuatilia dhuluma hiyo.

Aliwahakikishia wananchi hao kuwa malalamiko yao yatashughulikiwa na hatua muafaka kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa. Wakulima hao walikuwa wanataka kufidiwa kutokana na kupata hasara kuanzia kuandaa mashamba hadi kuotesha. “Tunataka kujua watatufidia je hasara tuliyopata?” alihoji mkulima Monika Gervasi.