Kairuki ‘awapa kadi ya njano’ maofisa wa madini

Muktasari:

  • Kairuki alisema hayo jana mkoani hapa wakati akifungua mafunzo ya kazi kwa viongozi na maofisa waandamizi wa Tume Madini walioteulewa hivi karibuni kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Morogoro. Waziri wa Madini, Anjela Kairuki amesema hatasita kutengua uteuzi wa ofisa yeyote wa madini au wa kazi wa migodi atakayeshindwa kufanyakazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kazi na kuwataka wawe wazalendo na kuepuka migogoro.

Kairuki alisema hayo jana mkoani hapa wakati akifungua mafunzo ya kazi kwa viongozi na maofisa waandamizi wa Tume Madini walioteulewa hivi karibuni kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Alisema yapo malalamiko yaliyowasilishwa wizarani kwake kuwa baadhi ya maofisa wamekuwa wakihujumu mfumo wa uombaji leseni za uchimbaji kwa kuzuia wengine kuomba leseni hizo.

“Wapo baadhi ya maofisa ambao wamekuwa wakizima mfumo wa uombaji leseni za uchimbaji kwa makusudi ili waombe wao halafu baadaye anakuja mtu mwingine anaambiwa tayari leseni imeshaombwa. Tumeshawabaini na hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” alisema.

Kutokana na malalamiko hayo, aliwaomba raia wema kutoa taarifa za ofisa yeyote wa wizara yake au Tume ya Madini atakayekuwa anamiliki leseni ya uchimbaji wa madini au uuzaji wa madini iwe kwa jina lake au jingine ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Waziri Kairuki aliwataka maofisa hao kusimamia uzalishaji wa madini katika migodi na kusimamia mauzo ya madini na mnyororo mzima wa madini kuanzia uchimbaji hadi usafirishaji kwenda nje ya nchi.

Aidha, aliwataka maofisa madini wa mikoa kuainisha maeneo ambayo wanayaona yanafaa kwa ajili wachimbaji wadogo ili wizara iyatangaze na kufanya utaratibu wa kuyagawa.

Pia, amewataka maofisa wa migodi kuandaa mpango kazi kuhusu usalama wa migodi ili kulinda mazingira pamoja na afya za watu.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Cliford Tandali alisema katika Wilaya ya Ulanga kuna changamoto ya utoroshaji madini hivyo kuiomba Serikali kujenga ukuta kama wa Mirerani ili kakabiliana na changamoto hiyo.

Tandali alisema Serikali inaweza kukusanya mapato mengi kutoka Ulanga kupitia madini lakini hali kwa sasa iko ndivyo sivyo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada alisema maofisa hao watajadili historia ya mabadiliko ya Sheria Madini tangu ukoloni ambako kulikuwa na changamoto mbalimbali za Sheria ya Ardhi zilizojitokeza na hivyo kulazimika kuzifanyia marekebisho.