Mahakama ya Rufani yainusuru CRDB kupoteza Sh97 bn

Muktasari:

  • Awali Mahakama Kuu iliiamuru kumlipa mdai mabilioni ya shingi

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imeinusu Benki ya CRDB kupoteza mabilioni ya shilingi baada ya kutengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyoamuru kumlipa Issack Mwamasika fidia ya Dola 42 milioni za Marekeni (zaidi ya Sh97 bilioni).

Mahakama hiyo imetengua hukumu hiyo baada ya kuridhika na hoja za rufaa za CRDB zilizowasilishwa na mawakili wake, Kesaria Dilip na Dk Alex Nguluma.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo lililoongozwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma akishirikiana na Stella Mugasha na Jacobs Mwambegele.

“Udhamini binafsi waliousaini na kuufunga si tu unawafunga kulipa deni la mjibu rufani wa tatu au kukabiliana na ukamataji wa mali zao,” alisema Msajili John Kahyoza aliyesoma hukumu hiyo na kuongeza:

“Lakini unampa mrufani mamlaka ya kisheria kukatalia hati za dhamana zinazohusiana na mkopo ambao mjibu rufani wa pili alishakamilisha kuulipa.”

Januari mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliiamuru benki hiyo kumlipa Mwamasika kiwango hicho baada ya kushinda kesi ya madai aliyoifungua na kampuni zake mbili, kufuatia mgogoro wa kibiashara ulioibuka baina yao.

Katika kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2012, wadai walikuwa ni Mwamasika ambaye ni mwenyekiti wa Mfuko wa Wadhamini wa Dar es Salaam International School (DISTF) na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya EDBP & GD Construction Co. Ltd.

Wadai hao waliiomba Mahakama Kuu imuamuru mdaiwa awalipe fidia ya Dola 205.6 milioni kwa maelezo kuwa, CRDB iliendelea kuzishikilia hati za mali zake alizoweka dhamana licha ya kumaliza deni lake hivyo kumfanya ashindwe kuchukua mkopo wa Dola 70 milioni (zaidi ya Sh158 bilioni) kutoka United Bank of Afrika (Uba).

Katika utetezi, CRDB ilisema iliamua kukatalia hati hizo zilizowekwa dhamana ya mkopo wa Sh350 milioni kwa DISTF, kwa kuwa kampuni nyingine ya Bugali ilikuwa haijarejesha mkopo wake wa Dola 8.5 milioni.

Ilidai kuwa Mwamasika aliweka udhamini binafsi kuwezesha kampuni yake kupata mkopo huo na hadi alipoomba kurejeshewa hati za dhamana ya mkopo wa DISTF, kampuni ya EDBP & GD Construction Co. Ltd ilikuwa inadaiwa.

Hukumu hiyo inasema kulingana na ushahidi uliopo, mkopo wa Dola 8.5 milioni uliotolewa Machi mosi 2012 ulipangwa kulipwa kwa awamu 60 kwa mafungu ya Dola 228,196 ambao ungemalizika Februari 28, 2017. Kupitia kwa mawakili wake, Profesa Mgongo Fimbo, Mpaya Kamara na Martin Matunda walidai kiwango cha fidia ya Dola za Marekani 6 milioni ambacho mahakama iliamuru mjibu rufani wa tatu alipwe (EDBP & GD Construction Co. Ltd) kilikuwa ni kidogo.