Mapato Acacia yaathiri halmashauri

Muktasari:

  • Kushuka kwa mapato hayo kunasababisha maendeleo ya halmashauri hiyo kudorora kutokana na miradi mingi kutegemea mapato ya ndani.

Nyang’hwale. Mapato ya ushuru wa huduma yatolewayo na mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu kwa Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita yameendelea kushuka kutoka Sh400 milion zilizotolewa Januari/Juni 2016 hadi kufikia Sh59 milion kwa kipindi cha Januari/Juni.

Kushuka kwa mapato hayo kunasababisha maendeleo ya halmashauri hiyo kudorora kutokana na miradi mingi kutegemea mapato ya ndani.

Akizungumza kwenye makabidhiano ya hundi ya fedha hizo kati ya halmashauri na uongozi wa mgodi wa Bulyanhulu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Mariam Chaurembo alisema hali hiyo ina athiri maendeleo ya halmashauri.

“Malengo yetu mwaka jana ilikuwa kukusanya Sh1 bilioni lakini tumekusanya Sh800 milioni tu, kushuka kwa mapato haya kunatufanya tutetereke lakini tunajipanga kwa vyanzo vipya vya mapato ili tuweze kufikia malengo,” alisema Chaurembo.

Akikabidhi hundi hiyo, meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, Benedict Busunzu alisema katika kipindi cha Januari hadi Juni ushuru wa huduma unaopaswa kulipwa na mgodi huo ni Sh181.1 milioni.

Alisema halmashauri ya Nyang’hwale imelipwa asilimia 33 ya fedha hizo, huku asilimia 67 sawa na Sh121.3 milioni ikilipwa halmashauri ya Msalala kwa kuzingatia makubaliano baina ya mgodi na halmashauri hizo mbili.

Alisema sababu za kushuka kwa mapato ni kutokana na kushuka kwa uzalishaji lakini kutokana na mazungumzo baina ya Serikali na Acacia yanayoendelea wana imani kurudi kwenye uzalishaji mkubwa.

Mkuu wa wilaya hiyo, Hamimu Gwiyama aliitaka halmashauri hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato vitakavyo ongeza mapato ya ndani wakati huu wanaosubiri hatma ya mazungumzo.