Serikali yajivunia miradi 20 ya ubia

Muktasari:

  • Hatua hiyo imechangia kusukuma maendeleo ya nchi kwa miaka 28 badala ya kutegemea bajeti ya Serikali pekee.

Tanga. Miradi 20 yenye thamani ya Dola 863.39 milioni za Marekani imewekezwa nchini kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Hatua hiyo imechangia kusukuma maendeleo ya nchi kwa miaka 28 badala ya kutegemea bajeti ya Serikali pekee.

Naibu katibu mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Suzan Mkapa (pichani) alitoa taarifa hiyo jana akifungua mafunzo ya PPP kwa maofisa wa wizara na taasisi za Serikali jijini Tanga.

Mkapa aliutaja mradi wa aina hiyo kuwa ni uendeshaji wa huduma za usafiri Dar es Salaam (Udart) awamu ya kwanza ambao upo hatua ya utekelezaji.

Naye mtaalamu wa PPP kutoka Benki ya Dunia, Edward White alipongeza kwa kufanikisha mpango huo ambao umezaa matunda kwa baadhi ya nchi duniani.