TBA yaijaza Hazina mabilioni

Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga

Muktasari:

  • Mabilioni hayo kwa mujibu wa mtendaji mkuu wa TBA ni kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30 mwaka huu

Dar es salaam. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wametoa gawiwo la Sh2 bilioni ikiwa ni asilimia 15 ya mapato yao  ambayo wameelekezwa kuirudishia Hazina.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la TBA kwenye maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema fedha hizo ni za mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30.

Amefafanua kuwa gawiwo hilo limetokana na utendaji kazi wa viwango vizuri na unaoaminika.

Amesema anajivunia kuwa na rasilimali ya watu iliyo bora ikiwamo wataalamu 83, wahandisi 73 na watafiti wa majengo 65.

"Cha kujivunia wataalamu wote hawa ni kutoka hapa nchini hakuna hata mmoja kutoka nje, baadhi yao walipata ujuzi nje ya nchi lakini wanafanya kazi hapa ndani,"amesema Mwakalinga.

Ameeleza kuwa wamepunguza gharama za ujenzi kwa kununua vifaa vyao vya kisasa ikiwamo magari, mashine ya kuchanganya zege na magari ya kusafirishia zege.

Ameitaja changamoto wanayokutana nayo kwenye utendaji wao kuwa ni hali ya hewa isiyotabirika. "Kwa mfano mradi wa Mloganzila, tulipouanza tu mvua zikaanza kunyesha.

Amesema hilo ndilo jambo linalowapa changamoto kwa sababu mradi inabidi usimame na kuanza kutoa matope.