TCB yajiandaa kutumbua majipu

Muktasari:

Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa TCB, James Shimbe aliyasema hayo juzi alipotembelea kiwanda cha uchambuaji wa zao hilo kilichopo Kata ya Bukoli wilayani hapa, Mkoa wa Geita.

Geita. Bodi ya Pamba nchini (TCB), imesema haitakuwa tayari kuwajibishwa kwa makosa ya wasambazaji wa mbegu mbovu za pamba na kuahidi kuwatumbua watakaobainika kuzisambaza.

Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa TCB, James Shimbe aliyasema hayo juzi alipotembelea kiwanda cha uchambuaji wa zao hilo kilichopo Kata ya Bukoli wilayani hapa, Mkoa wa Geita.

Alisema tatizo linalowakabili wakulima wa pamba ni kugawiwa mbegu mbovu ambazo wakipanda hazioti na mwishowe lawama huelekezwa kwenye bodi hiyo.

Meneja wa kiwanda hicho, Madan Mohan alisema waliagizwa na TCB kukusanya tani 800 za mbegu, lakini wameshindwa kutekelezeka kutokana pamba ya maeneo hayo kushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko fuzari.

Mkaguzi wa Pamba wilayani hapa, Venance Kankutebe alisema ugonjwa huo ulishambulia mashamba ya wakulima katika wilaya 13 za Kanda ya Ziwa na wamewaagiza wenye kampuni kutumia mbegu zilizoathiriwa kutengeneza mafuta ya kupikia.