TCB yakusanya Sh10 milioni kwa faini

Muktasari:

Pia, zaidi ya watu 10 wakiwamo wanunuzi katika Wilaya ya Itilima walitozwa faini ya Sh3.7 milioni, kutokana na kuchezea mizani na uchafuzi wa pamba.

Mwanza. Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Kanda ya Magharibi, imekusanya zaidi ya Sh10 milioni kwa kuwatoza faini baadhi ya wanunuzi na wakulima wa pamba kwa kuharibu mizani na kuchafua pamba na kusababisha kukosa ubora katika soko la zao hilo.

Pia, zaidi ya watu 10 wakiwamo wanunuzi katika Wilaya ya Itilima walitozwa faini ya Sh3.7 milioni, kutokana na kuchezea mizani na uchafuzi wa pamba.

Akizungumza jijini hapa jana, Kaimu Meneja wa TCB Kanda ya Magharibi, Buluma Kalidushi alisema hatua hiyo inatokana na uwapo wa malalamiko ya uchafu kwenye pamba inayonunuliwa.

Kalidushi alisema watu hao walikamatwa kati ya Julai na Agosti 5, kutokana na ushirikiano mzuri baina ya ofisi yake, watendaji na viongozi wa Serikali za vitongoji hadi wilaya.

“Watu hao wakiwamo wakulima wasiopungua 10 walikamatwa wilaya za Maswa, Meatu na Itilima mkoani Simiyu kati ya Julai hadi Agosti 5,” alisema Kalidushi.

Licha ya mambo mengine, gazeti hili lilitaka kufahamu iwapo Mahakama inayotembea iliyofufuliwa na TCB msimu huu wa ununuzi wa pamba iwapo imepata mafanikio au la. Alisema kutokana na hali hiyo, vituo vinne vimefutiwa leseni kwa kukiuka masharti na taratibu. “Watu 16 wakiwamo wakulima watatu walikamatwa wilayani Maswa, wakatozwa faini ya Sh50,000 kila mmoja kwa kuchafua pamba kwa kutia maji au mchanga,” alisema na kuongeza wanunuzi wanane walikamatwa Meatu na kutozwa faini ya Sh500,000 kila mmoja.