TTCL yarudi serikalini kwa asilimia 100

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo jana alipotembelea makao makuu ya TTCL Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Serikali imeirudisha mikononi mwake kwa asilimia 100 Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) baada ya kuilipa Kampuni ya Bhart Airtel ya India Sh14.9 bilioni iliyokuwa imeingia nayo ubia.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo jana alipotembelea makao makuu ya TTCL Dar es Salaam.

Alisema hatua hiyo ni mkakati wa Serikali wa kuiwezesha TTCL kujitegemea ili kuzalisha faida, kuimarisha miundombinu na kutoa gawio kwake.

“Tunawataka TTCL mjipange vizuri mjitangaze ili muwe kampuni kubwa na bora ya mawasiliano nchini,” alisema Profesa Mbarawa.

Alifafanua kuwa katika kuiongezea nguvu TTCL, Serikali itawapa kituo cha Kutunza Taarifa cha Kijitonyama (Internet Data Center) ili ikisimamie na kupata mapato.

Aliwataka wafanyakazi wa kampuni hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kutoa huduma bora na za uhakika wakati wote.

“Tumetumia fedha za mkongo wa Taifa kumlipa mbia mwenzenu Bhart Airtel ili kuiwezesha TTCL kumilikiwa na Serikali, changamoto inayowakabili sasa ni kufanya mabadiliko makubwa katika upande wa kutafuta masoko ili kuongeza idadi ya wateja na kufanya kazi kwa faida,” alisema Profesa Mbarawa.

Alifafanua kuwa katika kuijali TTCL, Serikali imeipa masafa ya 1,800 na 2,100 na itawaongezea ya 800 yatakayowawezesha kuwa na huduma ya 4G LTE yenye mtandao wenye kasi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete alisema wamejipanga kutoa huduma katika maduka makubwa, hospitali, stesheni za treni, mabasi ya mwendokasi na viwanja vya ndege vya miji mikubwa ili wateja wanufaike na huduma za mtandao huo.

Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura aliishukuru Serikali kwa fursa inazoipa kampuni hiyo na kumhakikishia Waziri Mbarawa kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo matokeo ya mkakati wa mabadiliko ya kibiashara yataanza kuonekana.