Tanapa, TRA mkoani Arusha kukusanya Sh617 bilioni

Muktasari:

Taarifa hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na taasisi hizo katika mkutano wa wadau wa utalii ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuzungumzia sekta ya utalii mkoani hapa na changamoto zake.

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoani Arusha wanatarajia kukusanya Sh617.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Taarifa hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na taasisi hizo katika mkutano wa wadau wa utalii ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kuzungumzia sekta ya utalii mkoani hapa na changamoto zake.

Mkurugenzi wa Utalii na Masoko wa Tanapa, Ibrahimu Mussa akiwasilisha mada katika mkutano huo, alisema katika bajeti ya 2016/17, Tanapa inatarajia kukusanya Sh187 bilioni kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato.

Mussa alisema kati ya fedha hizo, Sh142 bilioni zitatumika kwa matumizi ya kawaida ya uhifadhi na Sh23 bilioni kugharamia miradi ya maendeleo.

Meneja Huduma kwa Wateja wa TRA Arusha, Regina Mkumbo akitoa mada katika mkutano huo, alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, mamlaka hiyo inatarajia kukusanya Sh430.4 bilioni mkoani hapa.

Hata hivyo, alisema kati ya Julai na Agosti, mwaka huu, TRA Arusha imevuka lengo baada ya kukusanya Sh64.6 bilioni wakati lengo lilikuwa ni Sh63.1 bilioni.

Alisema hadi sasa wadau wa sekta ya utalii ndiyo wanaongoza kwa kulipa kodi mkoani hapa, akiwapo mwenyekiti wa chama cha Mawakala wa Utalii(Tato), Willy Chambulo na wanachama wake.

Awali, akifungua mkutano huo, Gambo aliwahakikishia wadau wa utalii kuwa mkoa umejipaga kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kuongoza kwa kuingiza mapato mkoani hapa.